Baadhi ya wadau wa malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya Mtoto wakiwa na watoto wanaolelewa katika kituo cha kijamii cha Malezi na Makuzi kilichopo Disunyara katika halmashauri ya Wilaya Kibaha Mkoani Pwani.
Na Julieth Ngarabali, Kibaha
MTAALAMU wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto Davis Gisuka amesema wazazi wenye tabia ya kuwafungia watoto wao kwenye mageti wakiamini kutochangamana na wengine ndio malezi bora wanatakiwa kubadilika na kuachana na utaratibu huo ambao unamnyima mtoto uhuru wa kujifunza.
Davis ambaye anatoka katika Shirika la Children in Crossfire (CiC)amesema watoto wanatakiwa kucheza na wengine na wakirejea ikibainika kuna mambo hayaendi vizuri ndio muda wa kuwarekebisha na watakuwa wanajifunza zaidi kuliko kuwafungia na kuwafanya kuishi kama goigoi mbele ya wengine.
“Kitendo cha kuwafungia ndani ya mageti kinawafanya waendelee kucheza wao kwa wao na ndugu wa nyumbani lakini wakitoka nje kuna mambo watajifunza kutoka kwa wengine na ni muda sahihi kwao kujifunza kupitia wengine” amesema Gisuka.
Ametoa somo hili baada ya kutembelea kituo cha kijamii cha Malezi na Makuzi kilichopo Disunyara halmashauri ya Wilaya ya Kibaha ziara ambayo iliandaliwa na Taasisi ya Anjita ambayo iliwahusisha pia wadau mbalimbali lengo likiwa ni kuhamasisha uwepo wa vituo hivyo kwa watoto wenye umri wa kuanzia miaka mitatu.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Pwani Rachel Chuwa amesema ili kuwa na Taifa bora lazima kuwekeza kwa watoto wakiwa bado wadogo na kwamba watoto wanatakiwa kulelewa vizuri ili wakue kiakili na kimwili wakiwa na maadili mema.
Chuwa amesema uwepo wa vituo vya malezi na makuzi unasaidia watoto kuanza kujitambua mapema na kuchangamsha akili kwani wanahitaji kufundishwa wakiwa bado wadogo kipindi ambacho wanaweza kushika vitu vingi na kuhifadhi akilini.
Alielekeza Wazazi wote wenye watoto kuanzia miaka mitatu kuhakikisha wanawapeleka kwenye vituo vya Malezi na Makuzi na kwamba kwa maeneo ambapo bado vituo vya aina hiyo havipo wananchi wanatakiwa kuungana na kuvianzisha.
Janet Christian kutoka Taasisi ya Anjita ameeleza kwamba wamekuwa wakifanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo ya kusaidia watoto wenye mahitaji maalumu.
Anjia ambayo inafanya kazi na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, imeshiriki katika kufufua kituo hicho kwa kuchangia vifaa mbalimbali ikiwemo vya michezo ambavyo vinahamasisha mtoto kupenda kwenda shule.
Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu Joel Mwakapala ameongeza kuwa vituo hivo vinatakiwa kuanzishwa nchi nzima na wazazi wawekeze zaidi kwa watoto wa miaka 0-8.
Mwaka 2015 Wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi iliboresha mtaala wa elimu ya msingi kwa kuanza na ule wa darasa la kwanza na la pili na umeweka mkazo katika kukuza stadi za awali za kusoma kuandika na kuhesabu (KKK) na kwamba ulienda sambamba na kuboreshwa kwa mtaala wa elimu ya awali mwaka 2016.