BARRICK NORTH MARA YAPONGEZWA KWA KUENDELEZA TASNIA YA MICHEZO NA KUINUA VIPAJI VYA VIJANA WILAYANI TARIME


Wachezaji wa timu za soka ya Kewanja FC na Mrito wakichuana vikali katika mechi ya fainali ya mashindano ya Kemanyanki Cup yaliyofanyika Nyamongo Tarime jana kwa udhamini wa Barrick North Mara kampuni ya Kemanyanki. Kewanja FC iliibuka mshindi kwa kuichapa Mrito FC kwa mikwaju ya penati 4-2.
Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara akiongea baada ya kumalizika mashindano hayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kemanyanki, Nicolaus Mgaya akiongea baada ya kumalizika mashindano hayo
Afisa Raslimali watu wa kampuni ya Kemanyanki,Celina Mkaro akisoma taarifa ya mashindano hayo

***
MBUNGE wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara ameupongeza Mgodi wa dhahabu wa Barrick North kwa jitihada inazofanya kuendeleza tasnia ya michezo wilayani Tarime kutokana na udhamini ambao imekuwa ikitoa kwa mashindano ya michezo mbalimbali wa vijana kwa kushirikiana na makampuni yanayofanya kazi kwenye mgodi huo, pia ameeleza kuridhishwa na ushirikiano unaooneshwa na Kampuni ya Barrick kwa kampuni za wazawa na jamii inayozunguka Mgodi huo.

Waitara aliyasema hayo wakati wa fainali ya mashindano ya soka ya Kemanyanki Cup yaliyoandaliwa na kampuni hiyo ya kitanzania ya Kemanyanki inayofanya kazi katika mgodi wa Barrick North Mara yalizozishirikisha timu 12 za vijana kutoka vijiji 11 vinavyozunguka mgodi huo uliopo Nyamongo wilayani Tarime, Mara.

Mechi ya fainali ya mashindano hayo - kati ya Kewanja FC na Mrito FC ilichezwa katika uwanja wa Shule ya Sekondari Ingwe iliyopo mjini Nyamongo jana .

Katika mchezo wa fainali ya Kemanyanki Cup uliokuwa na ushindani mkali, Kewanja FC iliibuka mshindi kwa kuichapa Mrito FC kwa mikwaju ya penati 4-2.

Kwa ushindi huo Kewanja ilitwaa kombe, medali, jezi na shilingi 800,000 huku Mrito ikipata jezi, medali na shilingi 450,000 na Nyangoto iliyoshika nafasi ya tatu ilipata medali, jezi na shilingi 300,000. Kemanyanki ni moja ya kampuni za wazawa zinazofanya kazi na Kampuni ya Barrick katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa kutoa huduma mbalimbali.

“Ninawapongeza vijana waliounda kampuni ya kizalendo ya Kemanyanki kwa kuamua kukileta kidogo walichonacho kwenye jamii. Lakini pia niwapongeze mgodi wa North Mara kwa ushirikiano wao wa kila mara, haya ndiyo tunayotaka yaendelee kufanyika,” alisema Mbunge Waitara ambaye alikuwa mgeni rasmi katika fainali hiyo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kemanyanki, Nicolaus Mgaya aliishukuru kampuni ya Barrick kwa kuona umuhimu wa kufanya kazi na kampuni za wazawa katika mgodi wa North Mara.

Mgaya alisema wananchi wanaoishi vijiji vinavyozunguka mgodi huo wana kila sababu ya kujivunia uwepo wa Kampuni ya Kemanyanki na mgodi huo kutokana na kuwatengenezea fursa za ajira na biashara.

Akizungumzia mashindano ya Kemanyaki Cup, Mgaya alisema yamewezesha vijana kuufahamu vizuri mgodi wa North Mara na faida zake kwa umma, lakini pia wameweza kubadilishana mawazo yenye manufaa katika maisha yao na jamii inayozunguka mgodi huo.

“Kemanyanki ni kampuni ya jamii ya vijiji vinavyozunguka mgodi, unapoiona Kemanyanki popote pale ujue ni mali yako,” alisema Mgaya na kuendelea:

“Tunataka kuibua vipaji ndani ya jamii, kudumisha ushirikiano, kutengeneza network (mtandao) katika jamii yetu na kutumia vizuri fursa zilizopo. Tunahitaji vijana wetu wawe ndio sehemu kubwa ya kuifaidi keki tunayoipata.”alisisitiza Mgaya.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464