RC MNDEME AWAAGIZA SUMA JKT KUONGEZA KASI UJENZI JENGO LA MAMA NA MTOTO HOSPITALI YA KAHAMA


RC MNDEME AWAAGIZA SUMA JKT KUONGEZA KASI UJENZI JENGO LA MAMA NA MTOTO HOSPITALI YA KAHAMA.

Na Marco Maduhu,KAHAMA

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme, amewaagiza SUMA JKT kuongeza kasi ya ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama, ili lianze kutoa huduma za matibabu.

Ametoa maagizo hayo leo Septemba 20,2023, wakati alipotembelea katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama kuona maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo la Mama na Mtoto.
Amesema ujenzi wa Jengo hilo kwa sasa upo asilimia 30, ambao ulipaswa hadi sasa kufikia asilimia 35 na kuwa nyuma asilimia 5,na unapaswa kukamilika 2025.

"Fedha za ujenzi wa Jengo hili la Mama na Mtoto siyo tatizo, sababu Rais Samia ameshatoa fedha hivyo hakuna sababu ya mradi huu kuchelewa kukamilika ndani ya wakati, nawaagiza SUMA JKT ongezeni kasi,muongeze wafanyakazi na mfanye kazi usiku na mchana,"amesema Mndeme.
Aidha, amesema Serikali inataka akina mama wajisikie raha wanapokuwa wakijifungua na kujifungua salama watoto wao, ndiyo maana inazidi kuboresha huduma za afya, na kuwaomba wananchi waendelee kumuunga Mkono Rais Samia ili aendelee kuwaletea maendeleo.

Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kahama Thomas Muyonga, amesema Jengo hilo ni muhimu katika kuhakikisha akina mama wanajifungua salama, na kusisitiza likamilishwe ndani ya muda.
Msimamizi wa mradi wa ujenzi huo kutoka SUMA JKT Mhandisi James Saimon, amemuahidi Mkuu huyo wa Mkoa kwamba watajenga usiku na mchana, na watakamilisha ndani ya muda na sasa ujenzi upo asilimia 30.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa wilaya ya Kahama Dk.Shani Mudamu, akisoma taarifa ya ujenzi huo, amesema utakamilika 2025 kwa thamani ya Sh.bilioni 6.7 na unatekelezwa na SUMA JKT.
Naoa baadhi ya akina Mama wa Kahama, wameipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha huduma za Afya na kuwasogezea huduma hizo karibu na makazi yao, na kuokoa Afya zao pamoja na kujifungua watoto salama.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme akizungumza na baadhi ya wagonjwa katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme akiwa ziara katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama kukagua ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464