NDOA ZA UTOTONI MASENGWA WILAYANI SHINYANGA ZA DHIBITIWA
Sheria ndogo zatungwa
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
TATIZO la Ndoa za utotoni limeendelea kushughulikiwa na viongozi wa Serikali pamoja na wadau wa maendeleo mkoani Shinyanga, ili kuhakikisha tatizo hilo linakoma kabisa na kubaki kuwa historia.
Mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa mikoa hapa nchini ambayo bado tatizo hilo la kuozesha watoto ndoa za utotoni lipo, na hata kusababisha kuharibu ndoto za maisha yao.
Kata ya Masengwa wilayani Shinyanga imekuwa ikikabiliwa na tatizo la watoto kuozeshwa ndoa za utotoni, na hata Mabinti kupelekwa kushiriki kwenye ndoa za Kimila Maarufu Bukwilima ili wakashiriki ngono na wanaume ambao humsindikiza Bwana harusi ili wapate bahati ya kuolewa.
Kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa idadi ya watu na Afya (TDHS) ya Mwaka 2015/2016, mwanamke mmoja kati ya watatu nchini Tanzania huolewa kabla ya kutimiza miaka 18, kadhalika utafiti huo unaonyesha kuwapo na ongezeko la asilimia 5 la ndoa za wasichana walio katika Rika Balehe (umri wa miaka 15-19) tangu utafiti wa awali mwaka 2010.
Mwandishi wa Makala hii amekuwa wakiandika Makala ambao zinahusu kudhibiti tatizo hilo la ndoa za utotoni mkoani Shinyanga, ikiwamo na Kata hiyo ya Masengwa ambayo ilikuwa imeathiriwa na tatizo la mabinti kuozeshwa ndoa za utotoni kupitia ndoa za kimila.
Mtendaji wa Masengwa wilayani Shinyanga Hussein Majaliwa, akizungumza katika mahojiano maalumu, anasema mikakati ambayo wamejiwekea katika kupambana na ndoa za utotoni, ni kutunga Sheria ndogo kuanzia ngazi ya vitongoji,vijiji hadi Kata, kwamba Marufuku ndoa yoyote kufungwa kijijini bila ya kupata kibali kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Anasema wamefanya hivyo sababu walikuwa wamejisahau kuwalinda Mabinti wadogo ambao wapo majumbani ambao hawasomi shule na wengine wakiwa wamemaliza darasa la Saba na kushindwa kuendelea na Masomo huku umri wao ukiwa chini ya miaka 18, ambapo wazazi huwaozesha kwa tamaa ya kupata mifugo.
Majaliwa anasema baada ya kuligundua tatizo hilo ndipo wakatunga Sheria ndogo ambayo licha ya kuwalinda wanafunzi ambao wapo shuleni pia itawalinda mabinti wadogo waliopo majumbani wasiozeshwe ndoa za utotoni bali wasubili hadi watimize miaka 18 ndipo waolewe.
“Katika kudhibiti tatizo la ndoa za utotoni hapa Masengwa tumetunga sheria ndogo ni marufuku harusi yoyote kufungwa bila ya kupata Kibali kutoka kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa ambao ni wenyeviti wa Vitongoji, Vijiji, au Mtendaji wa Kata,”anasema Majaliwa.
“Tumefanya hivi ili kumaliza kabisa tatizo hili la ndoa za utotoni sababu baadhi ya wazazi hushawishi watoto wao wafanye vibaya mitihani ya Darasa la Saba ili wapate Mwanya wa kuwaozesha kwa madai hawasomi shule huku wakiwa bado na umri mdogo, kwa tamaa ya kupata mifugo na kuharibu maisha ya mtoto,”anaongeza Majaliwa.
Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Masengwa wilayani Shinyanga Oliva Mayanza, anasema tangu kuanza kutumika kwa sheria hizo tatizo la ndoa za utotoni limepungua siyo kama miaka ya nyuma.
Anasema jamii nayo imeelimika na kutoa taarifa pale wanapoona mtoto akitaka kuozeshwa, na kwamba mwaka huu walipokea taarifa ya mtoto kutaka kuozeshwa lakini ndoa hiyo waliidhibiti haikuweza kufungwa na mwanafunzi kuendelea na masomo.
“Ndoa hizi za utotoni zimepungua sana hapa Masengwa siyo kama miaka ya nyuma, hii inatokana na utungwaji wa Sheria hizi ndogo na utolewaji wa elimu kwa jamii juu ya madhara ya kuozesha watoto, kwa takwimu tulizonazo hapa ofisini mwaka huu kulikuwa na ndoa ya mwanafunzi mmoja kutaka kufungwa tukaizuia,”anasema Oliva.
Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya wilayani Shinyanga Aisha Omary, anasema ndoa za utotoni ni kikwazo kikubwa cha kuharibu maisha ya watoto wengi wa kike katika maeneo ya vijijini.
Anasema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wamekuwa wakipambana kutokomeza ndoa hizo, kwa kutoa elimu pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria wazazi ambao huendekeza tamaduni za kuozesha watoto, na wamefanikiwa kuzipunguza.
“Ndoa za utotoni wilayani Shinyanga zimepungua, takwimu za mwaka jana zimefungwa ndoa tatu ambazo tuna taarifa nazo, na zenyewe tulifanikiwa kuzitibua, lakini miaka ya nyuma zilikuwa zikifungwa ndoa hadi 10 kwa mwaka, na chanzo cha ndoa hizi ni Mila na Desturi Kandamizi,” anasema Aisha.
Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Kata ya Masengwa Joyce Richard, anasema sheria ndogo na elimu ya madhara ya kuozesha ndoa za utotoni, imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la ndoa za utotoni ndani ya jamii.
Anasema pia tatizo la Mabinti kuhudhuria kwenye ndoa za Kimila maarufu Bukwilima, ambao huhamasisha mabinti kushiriki ngono na wanaume ambao wanamsindikiza Bwana harusi ili wapate bahati ya kuolewa sasa hivi halipo tena baada ya jamii kuelimika.
Mzee Maarufu kutoka Masengwa wilayani Shinyanga Juma Ngelela, anasema katika mapambano hayo ya kutokomeza ndoa za utotoni, elimu bado inahitajika kutolewa kwa jamii, ikiwamo na wazazi kuacha tabia ya kuwaogesha watoto wao dawa za mvuto wa mapenzi.
“Jamii kwa kiasi fulani elimu wamepata juu ya madhara ya kuozesha watoto, lakini elimu hii inahitaji kuwa endelevu pamoja na sheria ndogo kutiliwa mkazo, mzazi akikamatwa ana ozesha mtoto awajibishwe ipasavyo,,”anasema Ngelela.
Mchungaji wa Kanisa la PAG Edward Salamba, anaiamsha Serikali kwamba katika kudhibiti ndoa hizo za utotoni, wanapaswa kuwa makini sababu jamii imekuwa na mbinu nyingi ikiwamo kuweka mabibi harusi feki ambao wana umri dhidi ya miaka 18.
“Jamii inapaswa kuzingatia maandiko ya Mungu, Mtoto wa kike anastahili kupendwa na kulindwa, hivyo iache kuwaozesha ndoa za utotoni,”anasema Salamba.
Mwenyekiti wa Baraza la watoto Mkoa wa Shinyanga na Taifa Rafael Joseph, anawasihi wazazi kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kuwapatia haki zao za msingi, ikiwamo kuwapeleka shule na kuacha kuwabagua watoto wa kike na kuwaozesha ndoa za utotoni.
Amewataka watoto wanapokuwa wakiona viashiria vya kufanyiwa ukatili, watoe taarifa mapema kwa viongozi wa Mabaraza ya watoto, walimu hata viongozi Serikali za Mitaa ili hatua za haraka zichukuliwa na kuzia vitendo vya ukatili zikiwamo na ndoa za utotoni.
Mkurugenzi wa Shirika la WEADO ambalo linatetea haki za watoto, wanawake, na wazee mkoani Shinyanga, Eliasenya Nnko, anasema katika mapambano ya kutokomeza ndoa na mimba za utotoni wilayani Shinyanga, wanatekeleza mradi wa vunja ukimya zuia ndoa na mimba za utotoni, kwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya kuozesha watoto.
Anasema ili kutokomeza tatizo hilo la ndoa za utotoni jamii inapaswa kuelewa madhara ya kuozesha watoto katika umri mdogo, ndiyo maana wao kwa sasa wapo katika utekelezaji wa mradi wa kutoa elimu kwa wananchi juu ya kuacha vitendo vya ukatili ikiwamo kuozesha watoto na kuzima ndoto zao.
Kwa mujibu wa Takwimu zilizotolewa na Shirika la watoto Duniani (UNICEF) Mwaka 2012, Mkoa wa Shinyanga umetajwa kuongoza kwa tatizo la ndoa za utotoni kwa asilimia 59 ikifuatiwa na Tabora 58 ya tatu ni mara 55.