RC MNDEME AWATAKA WANAFUNZI WAKIUME WASIKUBALI KUITWA BABY

RC MNDEME AWATAKA WANAFUNZI WAKIUME WASIKUBALI KUITWA BABY

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme,amewataka wanafunzi wa kiume wasiige tamaduni za kigeni ambazo hazifai na kukataa kuitwa baby.

Amebainisha hayo leo Septemba 25,2023 wakati alipofika katika Shule ya Sekondari Oldshinyanga kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa vyumba 11 vya Madarasa, Mabweni 4 na Matundu 16 ya vyoo.
Amesema Rais Samia ametoa fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu, hivyo Shukrani ambayo wanafunzi watampatia Rais ni kusoma kwa bidii, kuwa na maadili mema na kuacha kuiga tamaduni mbaya za kigeni.

"Wanafunzi zingatieni maadili mema huo ndiyo ufaulu wenu, msiige tamaduni za kigeni, watoto wa kiume msikubali kuitwa baby," amesema Mndeme.
Aidha, amewataka pia wanafunzi wa kike wasikubali kurubuniwa na wanaume, bali wakatae na kujikita kwenye masomo zaidi na kutimiza ndoto zao.

"Wanafunzi wa kike na nyie msiikubali kuingia kwenye vishawishi timizeni ndoto zenu kwa kuvaa magauni manne, ambayo ni Sare za shule, Joho la Mahafali, Shela na Vazi la uzazi," amesema Mndeme.
Katika hatua nyingine Mndeme amewataka wanafunzi kuitunza Miundombinu ya shule hiyo, huku akimwagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, kuweka bajeti ya ujenzi wa uzio katika shule hiyo ili wanafunzi wawe salama.

Naye Mkuu wa Shule hiyo Malale Masali, akisoma taarifa ya ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo,amesema imeshakamilika kwa asilimia kubwa na mingine imeanza kutumika na gharama zake Sh.milioni 865.2.
Nao baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo,wameipongeza Serikali kwa ujenzi wa Miundombinu ya shuleni hapo na kuahidi watasoma kwa bidii.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme akiwa katika Shule ya Sekondari OldShinyanga.
Muonekano wa Baadhi ya Mabweni.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme akiwa katika Mabweni ambayo tayari yameshaanza kutumiwa na wanafunzi katika shule ya Sekondari OldShinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme (kulia) akiwa na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Johari Samizi na Mkuu wa Shule ya Sekondari OldShinyanga Malale Masali katika bweni la wavulana.
Muonekano wa baadhi ya vyumba vya madarasa.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme akiwa katika vyumba vya madarasa ambavyo tayari vimesha anza kutumika.
Baadhi ya vyoo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme akiwa katika Shule ya Sekondari OldShinyanga.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464