UWT SHINYANGA WAKANUSHA TAARIFA KUUNGANA NA MBOWE KUPINGA MKATABA WA BANDARI
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
UMOJA wa wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Shinyanga pamoja na CCM wamekanusha taarifa zilizotolewa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kupitia mitandao ya kijamii, kwamba wanawake Umoja huo Kata ya Didia wilayani Shinyanga, wameungana na Mbowe kupinga Mkataba wa Bandari.
Katibu wa siasa na Uenezi CCM Mkoa wa Shinyanga Richard Masele, amebainisha hayo leo Septemba 12, 2023 akiwa pamoja na viongozi wa UWT Mkoani humo.
Katibu wa siasa na Uenezi CCM Mkoa wa Shinyanga Richard Masele, (katikati) akiwa na Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Shinyanga Grace Bizulu, na Katibu wa UWT Mkoa Asha Kitandala.
Amesema taarifa ambazo zimeenea kwenye Mitandao ya Kijamii, kwamba wanawake wa UWT Kata ya Didia wilayani Shinyanga wameungana na Mbowe kupinga Mkataba wa Bandari siyo za kweli na zinapaswa kupuuzwa.
Amesema siku hiyo ya Agosti 27, UWT Taifa walikuwa na Mkutano wa hadhara Kata ya Didia, na Chadema nao walikuwa na Mkutano Kata hiyo katika eneo tofauti, kwamba hakuna hata Mjumbe Mmoja wa UWT aliyekwenda kwenye Mkutano wa Mbowe kwa ajili ya kumuunga Mkono kupinga Mkataba wa Bandari.
Katibu wa siasa na Uenezi CCM Mkoa wa Shinyanga Richard Masele.
“Mimi nilikuwepo huko Didia sikuona Mjumbe yoyote wa UWT kwenye Mkutano wa Mbowe, huo ni uongo na kukosa Sera za kuwaambia wananchi kwenye Mkutano yao, na kukalia maneno ya kuchafuana tu,”amesema Masele.
Aidha, amesema wana CCM wote wana muunga Mkono Rais Samia katika uwekezaji wa Bandari kwa ajili ya maendeleo ya Taifa na hakuna ambaye anampinga, na kutoa wito kwa Watanzania wamuunge Mkono Rais katika uwekezaji huo, ambao utakuwa na manufaa makubwa kwa Taifa na kupaa kimaendeleo.
Naye Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Shinyanga Grace Bizulu, amesema wanalaani kitendo hicho cha Chedema kuandika taarifa za uongo na kuuchafua Umoja huo na Mwenyekiti wao Taifa Mary Chatanda ambaye hata hakuwepo kwenye Mkutano wa Didia, bali ulikuwa ukiongozwa na wajumbe wa NEC wa Umoja huo ambao ni Nadra Rashid na Asia Hamis.
Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Shinyanga Grace Bizulu.
Amesema siku hiyo ya Agost 27 Mwenyekiti wa UWT Taifa Mary Chatanda, alikuwa amepangiwa kufanya ziara Kata ya Iselamagazi Pamoja na Solwa, lakini wanashaghaa kwenye taarifa ya Chadema kuona inasema UWT wamkimbia Mary Chatanda kwenda kupiga kura ya wazi kwa Mbowe kupinga Mkataba wa Bandari.
Katibu wa UWT Mkoa wa Shinyanga Asha Kitandala, naye ameeleza kusikitishwa na Chadema kuzusha taarifa za uongo pamoja kufanya fujo kwenye Mikutano ya Umoja huo, akidai kwamba kila wanapokwenda kufanya Mikutano yao, Chadema walikuwa wakiwafuata na kufanya Mikutano jirani nao hali ambayo ni hatari kiusalama.
Katibu wa UWT Mkoa wa Shinyanga Asha Kitandala.
Mjumbe wa Baraza Kuu la Wanawake Tanzania (UWT) kutoka mkoani Shinyanga Christina Gule, amesema katika ziara hiyo ya viongozi wa UWT Taifa, imekuwa na mafanikio makubwa kwao katika kuimarisha Umoja huo, na kumhakikishia Rais Samia atapata ushindi kwa kishindo katika uchaguzi Mkuu 2025 na wapo pamoja naye katika uwekezaji wa Bandari.
Mjumbe wa Baraza Kuu la Wanawake Tanzania (UWT) kutoka mkoani Shinyanga Christina Gule.
Aidha, katika taarifa ya Chadema iliyoenea kwenye baadhi ya Mitandao ya kijamii Agost 27, 2023 inasema’ Akina mama wa CCM waungana na Mbowe kupinga Mkataba wa Bandari Shinyanga.’ Taarifa ambayo imepingwa vikali.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464