KIKONGWE WA MIAKA 80 AHUKUMIWA KWENDA JELA MIAKA 30 KWA KUMNAJISI MJUKUU WAKE WA MIAKA 8 SHINYANGA


Na Kareny Masasy,

Shinyanga

MAHAKAMA ya wilaya ya Shinyanga imemuhukumu Luhende Heke (80) mkazi wa kijiji cha Ihapa kata ya Old-Shinyanga kwenda jela miaka 30 kwa kosa la kumnajisi mwijukuu wake (8) ambaye alikuwa akisoma darasa la kwanza.

Hukumu hiyo imetolewa leo na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya Yusuph Zahoro baada ya kusoma shauri la jinai kesi namba 56 ya mwaka 2023 ambapo alieleza mtuhumiwa alitenda kosa hilo mnamo tarehe 8/02/2023 na kumnajisi mtoto huyo baada ya kutoka shuleni na bibi yake akiwa ameenda shambani.

Hakimu Zahoro amesema kesi ya kubaka chini ya kifungu cha 130(1)na (2)(e) pamoja na kifungu cha 131( 3) cha makosa ya jinai sura ya 16 kama ilivyorejewa 2022 Mahakama imejidhisha kutokana na ushahidi uliotolewa na shahidi wa kwanza ambaye ni mtoto mwenyewe kudai kubakwa na babu yake.

“Kesi hiyo ilikuwa na mashahidi watatu mtoto mwenyewe alijieleza ,Mwalimu shule anayosomea na daktari aliyempima nakujaza PF3 ambapo Mahakama ilijirizisha pasipo na shaka kutokana na maelezo na vielelezo vilivyokuwa vikitolewa’’alisema Zahoro.

Hakimu Zahoro amesema upande wa utetezi wa mshitakiwa alikuwa na mashahidi watano ambapo shahidi wa kwanza ambaye ni mtuhumiwa alisema yeye hakutenda kosa hilo alikuwa kwenye mkutano wa hadhara na mtoto alikuwa akibembelezwa katika kutoa maelezo ya ushahidi.

Hakimu Zahoro amesema shahidi wa pili ambaye ni mke wake na mtuhumiwa alisema alimuona mwijukuu wake akitokwa na damu sehemu za siri alipomuhoji alimueleza alikutana na kijana mmoja ambaye alimuingizia vijiti lakini mume wake hakuwepo nyumbani.

Hakimu Zahoro amesema Shahidi wa tatu alidai hakuwepo nyumbani lakini alimuona babu yake akitokea kwenye kikao na shahidi wa nne na tano walieleza mtoto huyo aliwaeleza kuwekewa vijiti sehemu za siri na kijana ambaye hamfahamu ndiyo maana alivuja damu nyingi.

“Kutokana na maelezo ya mashahidi wote watano maelezo yao yalipingana na upande wa pili ambayo yalitolewa na mtoto mwenyewe kunajisiwa, mwalimu na daktari wa hospitali ya rufaa ya mkoa na mahakama bila kutia shaka na kuwepo kesi ya kujibu imetoa adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela na rufaa iko wazi”alisema Zahoro.

Mwendesha Mashtaka ambaye ni wakili wa serikali Mboneke Ndimubenya kabla ya kutolewa hukumu hiyo alisema mtoto huyo kisaikolojia ameharibika na hata kimasomo hafanyi vizuri tena aliomba mahakama itoe adhabu kali kwa mtuhumiwa ili iwe fundisho kwa wengine.

Wakili wa kujitegemea Emanuel Kalulu aliyekuwa mtetezi wa mtuhumiwa na hakuwepo aliwakilishwa na wakili John Kabudi katika kesi hiyo aliieleza mahakama kutokana na umri wake wa miaka 80 nakutegemewa na familia nani kosa lake la kwanza aliiomba mahakama impunguzie adhabu.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464