BUGANDO YAKAMILISHA UBORESHAJI KIWANDA CHA UZALISHAJI MAJI TIBA, KUZALISHA CHUPA 720 KWA SIKU

 

Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, Dk Fabian Massaga (Katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kiwanda cha uzalishaji wa Maji Tiba katika hospitali hiyo.

 ***
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando imekamilisha ukarabati wa kiwanda cha kuzalisha Maji Tiba kitakachokuwa na uwezo wa kuzalisha Chupa 720 kwa siku.

Awali kiwanda hicho ambacho kinazalisha aina zaidi ya 10 za maji tiba kilikuwa kinazalisha Chupa 400 kwa siku huku uboreshwaji huo ukiongeza uzalishaji wa maji hayo kwa matumizi ya ndani hadi kufikia asilimia 93.

Akizungumza leo kwenye makabidhiano na uzinduzi wa kiwanda hicho, Mfamasia katika Kitengo cha Maji Tiba Bugando, Deus Sinibagiye amesema uboreshaji wa kiwanda hicho ni endelevu huku akidokeza kuwa Kitengo cha Maji Tiba kinalengo la kuongeza uzalishaji wa maji hayo hadi Chupa 1,400 kwa siku.

"Kiwanda hiki kimeipunguzia taasisi gharama ya manunuzi ya maji tiba kwani sasahivi hapa Bugando, Chupa moja inatengenezwa kwa gharama isiyozidi Sh650 ambapo bei ya sokoni kama tungeenda kununua inaanzia Sh850 hadi Sh1,000," amesema


"Maboresho haya yamesaidia kupunguza gharama ya upatikanaji wa maji hayo kwa mwezi Agosti ambapo kitengo kilifanikiwa kuokoa zaidi ya Sh20 milioni kutoka kwenye Chupa 10,000 zilizotumika mwezi uliopita," ameongeza

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Bugando, Dk Fabian Massaga amewaomba wadau wenye nia ya kuwekeza katika uzalishaji wa maji tiba kuchangamkia fursa hiyo ambayo amesema lengo ni kutanua wigo na kuzalisha kwa ziada ili kusambaza kwenye hospitali nyingine za Kanda ya Ziwa.


"Tutaendelea kuboresha miundombinu ya uzalishaji wa maji tiba na vifaa tiba ili kuleta utoshelevu katika huduma zinazotolewa kwa wagonjwa. Huu ni utekelezaji wa ushauri uliotolewa na wataalam wa Mamlaka ya Chakula na Vifaa Tiba (TMDA) walipotembelea hospitali yetu," amesema

Dk Massaga amewataka wataalam na watumishi wa hospitali ya Bugando kutunza kiwanda hicho sambamba na kuzingatia weledi wanapozalisha ili kulinda afya za wagonjwa na watumiaji wa maji hayo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Afya Saidizi Bugando, Dk Cosmas Mbulwa amesema Bugando inapambana kuongeza mtaalam mmoja ili wafike nane ili kuwezesha uzalishaji ufanyike mara mbili kwa siku.
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, Dk Fabian Massaga (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kiwanda cha uzalishaji wa Maji Tiba katika hospitali hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, Dk Fabian Massaga akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuzindua kiwanda hicho
Wafamasia wakiendelea na uzalishaji wa Maji Tiba katika kiwanda kilichopo katika Kitengo cha Famasia cha Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando jijini Mwanza.
Mmoja wa Watumishi wa Kitengo cha Famasia Bugando akiandaa chupa kwa ajili ya kupakia Maji Tiba katika kiwanda cha Maji Tiba cha Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando
Maji Tiba katika hospitali hiyo. Kiwanda hicho kitazalisha Chupa 720 kwa siku.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464