Mratibu wa chanjo mkoa wa Shinyanga Timothy Sosoma
Na Kareny Masasy,
MPANGO wa chanjo hapa nchini ulianza mwaka 1975 kukiwa na chanjo 3 tu hadi kufikia mwaka 1980 chanjo zimekuwa zikiongezeka hadi kufikia chanjo 14 za aina tofauti tofauti zinazotolewa kwa binadamu mpaka sasa.
Chanjo ya Rotavirus inayotolewa kwenye mwili wa binadamu imelenga hasa watoto chini ya umri wa miaka mitano ambayo imeelezwa na wataalamu ni kinga dhidi ya ugonjwa hatari wa kuhara.
Katika kitabu cha programu jumuishi ya Taifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto PJT-MMMAM 2021/2022-/2025/2026 kinaeleza ugonjwa wa kuhara huathiri asilimia 12 ya watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Pia kunachangia hadi asilimia 50 ya utapiamlo kwa watoto na kusababisha watoto kutofikia hatua zao timilifu za ukuaji.
Kitabu hicho kinaeleza hatari ya magonjwa ya maambukizi miongoni mwa watoto imeongezeka kwa kaya chache huku asilimia 2.7 ya watu kwenye kaya wameripotiwa kutumia sabuni wakati wa kunawa mikono angalau mara mbili kwa siku.
Mkazi wa kijiji cha Ntobo halmashauri ya Msalala Pendo Robert anasema mtoto wake ana miezi nane amepata chanjo ya Rotavirus kwa njia ya matone ambayo inamzuia kuhara elimu amepewa na wataalamu wa afya na hajapata tatizo lolote.
“Tunapata elimu ya chanjo tukipeleka watoto kliniki na tunaelezwa tuhamasishane pia kuna matangazo huwa yanapita mitaani yanaeleza nakutaja watoto umri gani wanapata chanjo”anasema Robert.
Gloria Shija mkazi wa kijiji cha Ntobo mwenye mtoto wa miaka miwili anasema amempatia chanjo ya kuzuia kuhara na hajawahi kupata ugonjwa wa kuharisha mpaka kuishiwa maji.
Mkazi wa kijiji cha Ntobo Samson John anasema ipo elimu potofu baadhi ya wazazi wamekuwa wakidanganyana mtoto atakuwa mdumavu lakini wengi wameanza kuelewa tofauti na zamani.
Mratibu wa elimu ya afya kwa umma kutoka halmashauri ya Msalala Peter Ngazo anasema mtoto akianza kuharisha ataishiwa maji sababu atakwenda haja zaidi ya mara tatu kwa siku.
“Dalili ni kuharisha ni kichefu chefu, atatapika atapata homa na tumbo kujaa gesi au kuhisi tumbo kuchoma choma ,kuuma na kupoteza hamu ya kula matokeo yake kupoteza maji lakini akipewa chanjo vitu hivyo ataviepuka”anasema Ngazo.
Ngazo anasema upo uhusiano mkubwa kati ya chanjo na lishe kwani atakapo anza mtoto kuharisha kama hana lishe nzuri uwezekano wa kupata utapiamlo ni mkubwa sababu vitu vinavyomkinga mwilini havitakuwepo nakumfanya kudhoofika au kupoteza maisha.
Ngazo anasema maandalizi ya baadhi ya wazazi kuwapatia watoto chakula wengine hawanawi mikono na wanafuga kucha ikiwa kirusi kinatoka kwenye kinyesi na kupitia kwenye mikono na mdomoni.
Ngazo anasema baadhi ya wazazi wamekuwa wakinyonyesha wakati mwingine wanashika titi bila kunawa nakumfanya mtoto kuanza kuharisha.
“Mtoto akifikisha umri wa miezi sita anaanza kupewa chakula cha ziada na kadri akiendelea kukua anafundishwa kula mwenyewe hali ya usafi inahitajika zaidi ili kumuepusha na magonjwa ya kuhara”ansema Ngazo.
Mratibu wa chanjo halmashauri ya Msalala Bazil Kafunja anasema zipo chanjo zaidi ya tisa ambapo kuna chanjo ya Rotavirus zinatolewa kwa watoto kwa lengo la kumzuia kuharisha.
Kafunja anasema upo umuhimu wa watoto kupata chanjo umri mdogo mzazi asipofanya hivyo atamuweka mtoto kwenye hatari kwani wazazi wanashauriwa wazingatie maelezo ya wataalamu wapate chanjo zote ikiwemo chanjo ya Rotavirus
“Chanjo ni kumkinga mtoto kwani hawezi kujikinga mwenyewe na tunapompatia chanjo tunamhakikishia ulinzi wake imara wa kutopata maradhi na kupoteza maisha”anasema Kafunja.
Kafunja anasema uchafu au kinyesi ni chanzo cha kuhara kwa mtoto kinasababishwa na wazazi ambao hawazingatii suala la usafi wa mwili na mazingira wanayoishi ndiyo maana analindwa kwa chanjo akiwa bado umri mdogo wa kutojitambua.
Kafunja anasema mtoto asipopatiwa chanjo akiwa na miezi sita na mwaka mmoja na nusu anaweza kupewa chanjo zingine lakini siyo ya Rotavirus kwani zenyewe zinahitajika mtoto apatiwe kuanzia umri wa wiki sita hadi wiki 14.
Kafunja anasema hata takwimu za magonjwa ya kuhara kwa watoto zimepungua ambapo utolewaji wa chanjo ya Rotavirus kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano katika kampeni iliyoisha mwezi Juni halmashauri ya Msalala imefikia asilimia 138.
Mratibu wa chanjo mkoa wa Shinyanga Timothy Sosoma anasema chanjo ya Rotavirus imeweza kuwafikia watoto wenye umri chini ya miaka mitano 39512 sawa na asilimia 109 hadi kufikia Juni 2023.
Sosoma anasema malengo ya upataji wa chanjo hiyo kwa watoto ilikuwa kuwafikia watoto 39192 hivyo walihamasisha na kuvuka lengo.
Daktari bingwa wa watoto kutoka hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga Mwita Ngutunyi anasema watoto hawaugui sana kuharisha mpaka kulazwa wamekuwa wakiugua kawaida na kuishia kutibiwa katika ngazi za Zahanati au vituo vya afya.
Ofisa program wa chanjo kutoka wizara ya afya Lotalis Gadau anasema lengo la kutoa chanjo ni kujikinga na Maradhi mbalimbali yanayoambukizwa kwa njia ya hewa kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Gadau anasema chanjo ya Rotavirus inazuia kuhara kukali ilianzishwa mwaka 2013 baada ya mwaka 2012 kesi nyingi za watoto chini ya miaka mitano zilikuwa za kuhara baada ya kufanya utafiti mdogo.
“Mtoto alikuwa akipatwa na tatizo la kuhara kukali alikuwa anaishiwa maji hadi kufikia hatua ya kupoteza maisha lakini sasa kesi hizo hakipo tena”anasema Gadau.
Gadau anasema mtoto anajisadia kwenye poti badala ya kupeleka chooni kinatupwa shambani wakati mwingine mtoto kuchezea mdoli anakuwa akiuweka mdomoni huenda mdoli huo ukawa mchafu mtoto kupelekea kuharisha.
Gadau anasema hapa nchini watoto hupata chanjo ya Rotavirus kwa awamu tatu ambapo mwaka 2021 watoto zaidi ya Millioni 2.3 walipata chanjo na mwaka 2022 watoto Millioni mbili wamepata chanjo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Tanzania Demographic Health Suvey ( TDHS) ya mwaka 2015/2016 inaeleza kuwa asilimia 80 ya kaya hazina utaratibu mzuri wa usafi wa mazingira na utupaji wa kinyesi.
Shirika la afya duniani (WHO) lilieleza takribani watoto 450,000 hufariki kila mwaka duniani kote kutokana na virusi vya Rota vinavyoishi kwenye kinyesi cha binadamu kinachosababisha kuhara
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464