KISHAPU WAJIVUNIA MABILIONI YA RAIS SAMIA KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO KWA WANANCHI

KISHAPU WAJIVUNIA MABILIONI YA RAIS SAMIA KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO KWA WANANCHI

Na Marco Maduhu, KISHAPU.

MKUU wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude, amesema katika utawala wake Rais Samia, ametoa fedha nyingi wilayani humo ambazo zimetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi.
Amebainisha hayo leo Septemba 22,2023 wakati akizungumza katika Mkutano wake na waandishi wa habari, kwa kutoa taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha (2023/2024), na Miaka miwili na Nusu ya Utawala wa Rais Samia namna miradi hiyo ilivyotekelezwa.
Amesema kwa kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2021 hadi 2024 wilaya hiyo ya Kishapu ilipokea na kutumia kiasi cha fedha Sh,bilioni 40.4 kwa ajili ya kutekelezwa miradi mbalimbali ya maendeleo na miradi hiyo imesimamiwa vizuri na imekamilika na kutoa huduma kwa wanachi kama ilivyokusudiwa.

“Wilaya ya Kishapu tunatoa shukrani za dhati kwa Rais Samia kwa kutoa fedha nyingi ambazo zimetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Sekta ya Afya, Elimu, Maji, Kilimo,Mifugo,Mendeleo ya Jamii, Biashara na uwekezaji, Utawala Bora na TARURA,”amesema Mkude.
Amesema kwa upande wa Sekta ya Afya, wamefanikiwa kujenga Zahanati 6, Vituo vya Afya viwili, huku wakijenga kituo kingine Mwamalasa, pamoja na kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya majengo 11 katika Hospitali ya wilaya ya Kishapu, huku upatikanaji wa Madawa ukiwa ni asilimia 98 na kutoa huduma bora ya matibabu kwa wananchi.

Amesema katika Sekta ya Elimu wamejenga shule mpya za Msingi pamoja na kukarabati miundombinu ya elimu ikiwamo na ujenzi wa matundu vya vyoo na kuimarisha hali ya usafi na mazingira shuleni.
“Katika Sekta ya Elimu wilaya ya Kishapu tumejenga shule Mpya 2 za Msingi zenye jumla ya vyumba vya madarasa 32 na Majengo mawili ya utawala, kukamilisha ujenzi wa Shule Shikizi 5, Sekondari tumekamilisha vyumba vya Madarasa 121, Matundu ya vyoo 45 na kuweka miundombinu ya Maji,”amesema Mkude.

Amesema pia wamejenga mabweni Matano, nyumba 8 za Walimu, Chuo cha VETA na wameanza kudahili wanafunzi na kutoa mafunzo ya ufundi kwa vijana.
Kwa upande wa Kilimo na Mifugo wametekeleza shughuli mbalimbali pamoja na kununua mbegu za malisho kilo 70 kwa ajili ya uanzishwaji wa mashamba darasa mwili ya malisho, utoaji wa chanjo Ng’ombe 88,000, uchimbaji mitaro ya umwagiliaji kilomita 20, na ununuzi wa vifaranga vya samaki 12,000 na kupandikiza katika Bwawa la Songwa.

Amesema pia kupitia Programu ya EBBAR, wamejenga Malambo matatu, na wamekarabati Lambo Moja na kuendeleza ujenzi wa kituo cha unenepeshaji mifugo na ujenzi wa Kiwanda cha kuchakata bidhaa za ngozi katika kijiji cha Kiloleli.
Kwa upande wa Sekta ya Maji kutokana na utekelezaji wa miradi hiyo kupitia RUWASA, wameweza kufikia asilimia 56 ya upatikanaji wa maji vijijini ikiwa ni ongezeko la asilimia 2.5, na kufikia asilimia 53 mjini kwa ongezeko la asilimia 10.

Amesema ujenzi wa miundombinu ya Barabara,Madaraja na Makalavati kupitia TARURA waliingia Mikataba 8 ya matengenezo ya Barabara na Wakandarasi yenye thamani ya Sh.bilioni 2.2, pamoja na kufungua Barabara mpya Kilomita 41.
Idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imeweza kuongeza chanzo cha mapato kwa kujenga vibanda 42 vya biashara na vyoo katika Stendi ya Mabasi Maganzo.
Amesema wilaya hiyo pia imetekeleza afua za lishe ili kupunguza tatizo la udumavu kwa watoto, pamoja na kutoa mikopo ya asilimia 10 ambazo Nne kwa wanawake na Vijana na asilimia 2 kwa watu wenye ulemavu.

Aidha, amesema kwa upande Idara ya Rasilimali watu utawala bora wametekeleza shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba ya Mkuu wa wilaya, Katibu Tarafa Mondo, Ofisi ya Mkuu wa wilaya, ununuzi wa Gari 2 kwa ajili ya Idara ya Elimu Sekondari na Fedha pamoja na Pikipiki 39.
Ametaja pia kiasi cha fedha Sh.bilioni 6.0 kimetumika katika mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za idara hiyo wakiwamo na walengwa wa TASAF.

Katika hatua nyingine imeitaka Ofisi ya Mkurugenzi kwa kushirikiana na Wakuu wa Idara kuendelea kusimamia vizuri fedha hizo za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ambazo zimekuwa zikitolewa na Rais Samia, na miradi hiyo ikamilike na kutoa huduma kwa wananchi.

Nao baadhi ya wananchi wa Kishapu wameipongeza Serikali kwa kuwatekelezea miradi mbalimbali ya maendeleo wakidai kwamba miaka ya nyuma wilaya hiyo ilikuwa nyuma kwa kila kitu na walikuwa na shida nyingi hasa ukosefu wa maji, huduma za Afya na ubovu wa miundombinu ya barabara lakini sasa hivi huduma hizo zipo karibia kila mahali.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464