Zahanati ya Saeni yazinduliwa kuokoa vifo vya mama na mtoto
Julieth Ngarabali ,Kibaha
WAJAWAZITO na watoto wa umri wa miaka 0 mpaka nane katika kata ya Misugusugu mjini Kibaha wameondokana na adha ya kusafiri umbali wa zaidi ya kilomita 20 kufuta huduma za afya huko Mlandizi Kibaha Vijijini kufuatia kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa zahanati ya kisasa ya Saeni na kuanza kutoa huduma zote ikiwemo ya afya ya uzazi.
Wajawazito hao ni miongoni mwa Wananchi takribani 14,000 wanaoishi kwenye mitaa mitatu ya Saeni, Zogowale na Jonung'ha katika kata ya Misugusugu mjini Kibaha ambao awali walikabiliwa na changamoto ya kutembelea umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Akizindua kuanza huduma za afya katika zahanati ya Saeni Mbunge jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka amesema kuanza kwa huduma hizo ni jitihada za Wananchi wa maeneo hayo kujitolea nguvu zao wenyewe ikiwemo halmashauri na Serikali.
Koka amesema wananchi walipochoshwa na adha ya kutembea umbali mrefu walitafuta eneo la ujenzi wa mradi huo ambapo katika kuwaunga mkono alichangia sh Milioni 6.5 kwa ajili ya kununua mifuko ya saruji ya kuanzia ujenzi huo na wadau wengine wakaunga jitihada hizo.
" Mnakumbuka wakati nilipoomba ridhaa ya kuwa Mbunge wenu mliniambia mna shida ya maji, barabara na zahanati niliwapigia magoti kuwaomba kuwa tutazitatua na kweli tumeshirikiana halmashauri pamoja na Serikali ya CCM leo tumekamilisha vyote.
Mbunge Koka amesema zahanati ndio hii imefunguliwa nani mkombozi mkubwa hapa kwenye vijiji vyetu itasaidia wajawazito kuwahi matibabu na hata watoto kuhudhuria kliniki .
Mbunge Koka alibainisha lengo lake kubwa ni kuwatumikia wananchi hivyo atahakikisha anaendelea kushirikiana nao jimboni humo kwenye sekta zote ili waweze kuondokana na kero ambazo wamekuwa wakizipata.
Awali mganga mfawidhi wa halmashauri ya mji Kibaha Peter Nsanya amesema mradi wa Ujenzi zahanati hiyo mpaka kukamilika umegharimu sh Millioni 181 zilizotokana na nguvu za wananchi ikiwemo mfuko wa mbunge ikiwemo halmashauri na Serikali kuu.
"Mradi wa ujenzi huo utaweza kusaidia zaidi hasa kwa upande wa huduma za mama na mtoto ambao walikuwa wanapata shida ya kusafiri umbali mrefu kuzifuata huko Mlandizi huduma za afya hata hivyo bado upo upungufu wa viti " amesema dk Nsanya.
Aidha Diwani wa kata ya Misugusugu Upendo Ngonyani amemshukuru Mbunge Koka kwa namna anavyoshirikiana na Wananchi kuzitatua changamoto zilizopo na pia kutekeleza ilani ya CCM kwa vitendo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464