DC azindua kampeni ya “TUWAJIBIKE”
Na Kareny Masasy,Kahama
MKUU wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga Mboni Mhita,amezindua kampeni ya Tuwajibike yenye kauli mbio “Risti yako maendeleo yako”ambayo itakwenda sambamba na utoaji wa elimu ya matumizi sahihi ya mashine ya kieletroniki (EFD) kwa wafanyabiashara wadogo, wakati na wakubwa.
Aidha, kampeni hiyo itaendeshwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) Mkoa maalumu wa kikodi Kahama, na kila mteja na muuzaji wanatakiwa kuhakikisha wanadai na kutoa rista kwa kila bidhaa inayouzwa ili serikali isipoteze mapato yake.
Mhita amezindua kampeni hiyo jana tarehe 21/09/2023 katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama kwa kuhudhuriwa na Maaofisa kutoka TRA, Wakuu wa idara za halmashauri ya Ushetu, Msalala na Manispaa hiyo pamoja na chemba ya wafanyabiashara.
Amesema, wafanyabiashara wanatakiwa kuwajibika kutoa risti kwa kila biashara anayofanya ili kuepuka adhabu ambazo zinaweza kujitokeza pale atakapobainika kutotoa risti kwa mteja, kwani faini na adhabu zinasababisha kushusha mitaji yao.
“Hakikisheni kila biashara inayofanyika inakwenda sambamba na risti yake, kampeni hii baada ya kutoa elimu ya matumizi ya EFD tutaanza kuchukua hatua kwa wale ambao hawatoi wala kudai risti…..Hatutapenda kuona serikali inakosa mapato yake huku tunaweza kuzuia hili”Anasisitiza.
Kaimu Meneja wa TRA mkoa wa kikodi Kahama Wisaka Kamwamu amesema, wamejipanga vema kudhibiti wale wafanyabiashara wanaotoa risti ambazo ni feki, wakiziangalia katika mifumo yao hazisomi, na atakayebainika atafunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara Charles Machali amesema, kila katika vikao anavyofanya na wafanyabishara wake amekuwa akisisitiza suala la utoaji wa risti za EFD halali na mpaka sasa hajapata kesi yoyote dhidi yao na atakapobainika mfanyabiashara wake anafanya udanganyifu atamripoti.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464