UKWELI USIPINDISHWE ILI KUMLINDA MTOTO

MAHAKAMA KUU KANDA YA SHINYANGA

Na  Kareny Masasy

KWELI inasikitisha kwa umri wa mzee Luhende Heke (80) mkazi wa kijiji cha Ihapa kata ya Old-Shinyanga  ambaye Mahakama ya Wilaya ya Shinyanga imemkuta anahatia ya kunajisi mwijukuu wake wa darasa la kwanza  na kufungwa miaka 30 jela.

Mzee huyo ki umri katika familia au ukoo akitegemewa kuwa mstari wa mbele kukemea vitendo vya ukatili vinavyofanywa na wengine wasio na maadili  lakini imekuwa kinyume.

Jamii ya wilaya ya Shinyanga na maeneo mengine itambue kuwa ipo  haja ya kumlinda mtoto kwa mujibu wa sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

Kupitia sheria hiyo Kifungu namba 65 kinaeleza mtoto anatakiwa kulindwa na jamii nzima sio mzazi pekee kumbe hata huyo babu alipaswa awe mlinzi wa mtoto huyo siyo adui wa kumfanyia unyama.

Hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya Shinyanga Yusuph Zahoro anasema  mtoto huyo alisikilizwa zaidi ya mara tano akirudia maneno hayo hayo  bila kupindisha na kumtaja babu.

“Upande wa mashahidi watano wa  mtuhumiwa walikuwa wakimtetea babu  na hakuna aliyemtetea mtoto lakini  Sheria  inatambua mtoto awe ametaka mwenyewe  au amemlazimisha  bado ni kosa la jinai sababu kinachoangaliwa hawezi kujisimamia”anasema Zahoro..

Zahoro anasema kunajisi au kubaka katika sheria kipo kwenye kifungu cha 130 (1)na (2)(e) pamoja na 131 (3) cha makosa ya jinai sura 16 kama ilivyorejewa 2022.

Mwendesha Mashitaka wilaya  ya Shinyanga ambaye ni wakili wa serikali  Mboneke  Ndimubenya  anasema Kucheleweshwa kwa kesi  ni mojawapo ya  watuhumiwa kuanza kujipanga kwa kuharibu kesi  kwa matokeo ya humfundisha mtoto kugeuza ukweli na ndicho kilichotokea  kwenye kesi hii.

Familia wamemuacha mtoto peke yake  akijitetee mwenyewe wote walijikita kumtetea babu ambaye  ni mtuhumiwa  aliyefanya kitendo cha kumnajisi mtoto.

“Familia bila kufahamu mtoto huyo alipata maumivu makali, ameharibiwa vibaya ameachiwa kovu la kidonda  huenda hata magonjwa  hivyo jamii inatakiwa ibadilike itoe ushahidi wa kweli”anasema Mwendesha Mashtaka.

Mwendesha Mashtaka Mkoa wa Shinyanga Ajuaye Zegeli anasema  jumla ya watoto 139 wamelawitiwa na kubakwa au kunajisiwa kwa  kipindi cha miezi sita.

Zegeli  anasema   wamesikiliza kesi 84 za ubakaji au kunajisiwa na ulawiti ambazo ni za kuanzia mwezi Juni 2022 hadi Desemba 2022.

Zegeli anasema  kuanzia Desemba 2022 hadi Februari 2023 wamesikiliza kesi 55 ambazo zote ni za ulawiti na ubakaji.

Zegeli  anasema  katika Mkoa wa Shinyanga hali ya ulawiti na ubakaji imekithiri na wanaofanya vitendo hivyo ni wazazi wa kiume na ndugu wa karibu.

 “Shida  kubwa wanapo kamatwa watuhumiwa watoa ushahidi wanakwepa kutoa ushahidi kwa sababu ni ndugu wanayamaliza huko huko na watuhumiwa wanaachiwa huru wanarudi kuendeleza ubakaji na ulawiti”anasema Zegeli.


Anasema "Kwa kweli hali ni mbaya   inasikitisha  kwani wengi wanaofanya matukio haya ni ndugu na wazazi wenyewe wanawabaka watoto wa kike na kuwalawiti, wengine wanakuwa na imani za kishirikina.

 Zegeli anasema ili vitendo hivi visiendelee elimu itolewe kuanzia makanisani misikitini, ili wananchi wasiogope kutoa ushahidi wale wale ndio watakuwa wanarudi na kuendeleza ukatili huu.
 Zegeli  anashauri  serikali ijenge nyumba ya kuwahifadhi wahanga wanaofanyiwa ukatili na watoa ushahidi kwa ajili ya kusubiri kesi inasikilizwa kuliko kurudi nyumbani ambapo wanaporudi huko wanabadilika kwa kufundishwa na vitisho.

 Zegeli anasema hali inavyokuwa  ndugu kwa ndugu wanakataa  nakuelewana mtoto ataje mtu mwingine lakini wakikaa sehemu moja na kesi ikaendeshwa kwa haraka watatoa ushahidi na mtuhumiwa atapewa adhabu yake.

Mratibu wa Dawati la jinsia na watoto mkoa wa Shinyanga mrakibu Mwandamizi wa jeshi la polisi Monica Venance  anasema kwa kweli Mkoa wa Shinyanga una matukio mengi ya ukatili.

 "Tuwaomba wanawake wapaze sauti wanapofanyiwa ukatili wao na watoto  waje kwenye vyombo vya sheria kwani ni wachache tu wanaokuja katika dawati la jinsia” anasema Venace.

Ofisa ustawi wa jamii mkoa wa Shinyanga  Lyidia Kwesigabo anasema  watoto wanaopata changamoto  kama hizo serikali ya mkoa inawapeleka mahali ambapo wanahifadhiwa bila ndugu kufahamu  na kupewa ushauri nasaha ili kurudi katika hali zao za kawaida.

“Huyu mtoto wakati kesi ikiendelea alipelekwa sehemu maalum  (jina limehifadhiwa) kwaajili ya kurudishwa kwenye hali yake  na huko amekutana  na watu wa saikolojia kwaajili ya kumuweka sawa natumaini amekuwa vizuri na anaendelea na masomo”anasema Kwesigabo.

Mtaalamu wa malezi na makuzi ya watoto kutoka  Children in crossfire( CiC )Davis Gisuka anasema  mtoto anaakili nyingi za kuweza kutambua mtu anayemfanyia matendo mabaya na maumivu anayoyapata   bila kuwekwa kisaikolojia anaweza kwenda na hali ya hofu nay eye kulipiza kisasi pindi akiwa mkubwa.

Baadhi ya wananchi mkoa wa Shinaynga Hamida Yahaya na Cesilia Matomi wanalieleza  tukio hilo kwa hisia tofauti kwa kulilinganisha na umri wa  mzee huyo   wanadai  hizo ni imani za kishirikina mtoto huyo umri alionao  alipaswa kulindwa.

Mussa Dokola anasema mtoto akienda kuishi mbali na familia yake nayo ni changamoto sawa na kumpoteza  hivyo jamii inatakiwa ibadilike  suala la kumlinda mtoto ni lalazima.

Ripoti ya shirika la kimataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) ya mwaka 2011 inayohusiana na ukatili dhidi watoto  ambapo imeeleza   Tanzania ni chanzo muhimu cha takwimu .

Ripoti hiyo inaonyesha  msichana mmoja kati ya watatu na mvulana mmoja kati ya watatu wanapitia aina mbalimbali za ukatili  wa kingono kabla hawajafikisha miaka 18 ambapo robo tatu ya  watoto wameripotiwa wanafanyiwa ukatili kupitia ndugu wa karibu na familia

Mwisho.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464