Na Mwandishi wetu -Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali amesisitiza kuwa utunzaji wa kumbukumbu na Nyaraka za Serikali ndio msingi mkuu wa Taifa katika uendeshaji wa shughuli zote za Taasisi.
Amesema hayo leo septemba 13, 2023, wakati akifungua mafunzo ya maadili katika utumishi wa Umma kwa watumishi wa Taasisi ya Uhamasishaji wa Uwazi na Uwajibikaji Katika Rasilimali Madini , Mafuta na Gesi asilia (TEITI), yanayofanyika kwa siku mbili jijini Dodoma.
Amesema kuwa, ana matumaini kila mtumishi wa taasisi hiyo atapata uelewa kuhusu Kanuni na maadili ya Utumishi wa Umma yatakayo mpelekea kujua haki na wajibu wake wakati akitekeleza majukumu yake sehemu ya kazi.
“Ndugu Washiriki, kumbukumbu na Nyaraka za Serikali ndio msingi mkuu wa Taifa letu katika uendeshaji wa shughuli zote za Taasisi. Uzalishaji, utumiaji, utunzaji na uteketekezaji sahihi wa kumbukumbu na nyaraka za Serikali ni jambo la msingi na la kuzingatiwa na watumishi wote.
Ni muhimu kufuata na kuzingatia miiko ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka pamoja na kuzingatia usiri na utengano sambamba katika matumizi yake” amesema Mahimbali.
“Ili Utumishi wa Umma uwe wenye ufanisi na wa kuheshimika. Watumishi wanapaswa kuzifuata Kanuni za Maadili ya Utumishi pamoja na kuwa na tabia na mwenendo unaozingatia Sheria, Kanuni na Miongozo katika Utumishi wa Umma" ameongeza Mahimbali.
Katika hatua nyingine, Mahimbali amewaahidi watumishi wa TEITI kuwa Wizara itawaboreshea maslahi ili kufanya kazi katika mazingira bora na yenye hadhi ya utumishi ya umma.
Pia, akitoa salaam kutoka kwa Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde, Mahimbali amesema kuwa waziri anawasihi kuzingatia mafunzo hayo kwa kila mada itakayo tolewa na wataalam kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma ili kuongeza ufanisi katika utendajikazi wa kila siku.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa TEITI, Mariam Mgaya amesema kuwa uwepo wa taasisi hiyo unasaidia wananchi kujua uwazi na uwajibikaji sambamba na kuziba mianya ya rushwa kwasababu wananchi wanakuwa na taarifa za kutosha kuhusu shughuli za uendeshaji na usimamizi wa rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia.
Akizungumzia juu ya majukumu ya taasisi hiyo Mariam amefafanua kuwa TEITI inajukumu la kuweka mahusiano mazuri baina ya Serikali, Kampuni na Wananchi katika sekta zote za rasilimali madini ,mafuta na Gesi asilia.