Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Dkt Ally Laay (wa pili kushoto) akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wa pili kulia) wakionyesha mkataba wa mkopo wa dola za Marekani milioni 150 uliowezeshwa na Benki ya Intesa Saopaulo na Benki ya Investec. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Mikopo ya Pamoja Intesa Sanpaolo, Gustaaf Eerenstein na Mkuu wa Masuluhisho ya Mikopo kwa Afrika kutoka Investec Bank, Rowan King.
Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Dkt Ally Laay (kushoto) akimshuhudia Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akisaini mkataba wa mkopo wa dola za Marekani milioni 150 uliowezeshwa na Benki ya Intesa Saopaulo na Benki ya Investec. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Masuluhisho ya Mikopo kwa Afrika kutoka Investec Bank, Rowan King pamoja na Mkurugenzi wa Mikopo ya Pamoja Intesa Sanpaolo, Gustaaf Eerenstein.
======== ====== =======
Dar es Salaam. Tarehe 17 Oktoba 2023: Benki ya CRDB imesaini mkopo wa dola za Marekani milioni 150 zitakazotumika kuwakopesha wateja wakubwa waliowekeza kwenye sekta tofauti za uchumi.
Mkopo huo wa kimataifa (international syndicated term facility) umechukuliwa kwenye soko la kimataifa la fedha ambako Benki ya Intesa Sanpaolo na Benki ya Investec zimeshirikiana kufanikisha mchakato huo uliovutia wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Akizungumza kwenye hafla ya kutia saini mkataba huo iliyofanyika jijini hapa, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema mpaka kuupata mkopo huo wa kimataifa, mambo mengi yamezingatiwa ikiwamo kukopesheka kwa benki, uthabiti wa menejimenti ya benki, uendeshaji wake kibiashara na pia tathmini ya uimara na uthabiti wa Benki unaofanywa na taasisi mahsusi za kimataifa kama Moody’s iliyoipatia Benki daraja B1
“Benki yetu imefanikiwa kupata kiasi kikubwa cha mkopo wa fedha za kigeni kutoka soko la kimataifa. Ni mafanikio yanayodhihirisha imani waliyonayo wawekezaji wa kimataifa kwetu kutokana na mfumo wetu mzuri wa uendeshaji biashara, kukopesheka kwetu na uchumi imara wa nchi yetu, Tanzania,” amesema Nsekela.
Akieleza mafanikio waliyoyapata, Nsekela amesema benki ilituma maombi ya kupata mkopo wa dola za Marekani milioni 50 lakini wingi wa wawekezaji waliojitokeza ulivuka malengo kwa asilimia 404 kwa kuwa dola za Marekani milioni 202 zilipatikana.
Hata hivyo, amesema licha ya fedha za ziada kukusanywa, Benki ya CRDB imechukua dola za Marekani milioni 150 tu sokoni ambazo ilizieleza ndani ya maombi yake ya awali.
“Katika utaratibu huu wa international syndicated facility, taasisi inayohitaji fedha kama ilivyokuwa kwetu Benki ya CRDB, anawasilisha ombi kwa shirika la fedha la kimataifa linalotambulika ambalo hulifikisha kwa wawekezaji tofauti wanaotaka kuwekeza Afrika. Kila mwekezaji, kulingana na anavyoitathmini taasisi husika inayoomba mkopo huo, husema yupo tayari kuwekeza kiasi gani kati ya kinachoombwa. Hii ndio maana kiasi kilichokusanywa kilikuwa kikubwa kuliko tulichoomba. Tulieleza kuwa iwapo kiasi kitazidi, uwezo wetu utakuwa ni kuchukua mara tatu ya kiasi tulichoomba,” amesema Nsekela.
Katika kiasi hicho ambacho Benki ya CRDB imekichukua kutoka wawekezaji wa nje wanaojumuisha kutoka Afrika Kusini, Italia, Mauritius, Misri, Ujerumani, Uingereza na Mashariki ya Mbali, dola za Marekani milioni 122 zitalipwa ndani ya mwaka mmoja na dola za Marekani 28 milioni zitarejeshwa ndani ya miaka miwili.
Benki ya CRDB ni taasisi ya kwanza ya fedha nchini kutathminiwa na Moody’s na kupewa daraja la juu hivyo kuingia miongoni mwa benki 10 za biashara ambazo ni rafiki kuwekeza barani Afrika. Kwenye tathmini yake, kampuni ya Moody’s imeipa Benki ya CRDB daraja B1 ambalo ni la juu zaidi kupewa taasisi ya fedha kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kwenye mkutano huo, Mkuu wa Masuluhisho ya Mikopo kwa Afrika wa Benki ya Investec, Leanne Large amesema “wingi wa wawekezaji waliovutiwa kuwekeza fedha zao katika Benki ya CRDB unadhihirisha kukua na kuimarika kwa benki hii pamoja na ushawishi wake katika uchumi wa Tanzania. Benki ya CRDB inakopesheka zaidi na wawekezaji wengi wanaiamini kufanya nayo biashara.”
Mkurugenzi wa Mikopo ya Pamoja wa Benki ya Intesa Sanpaolo, Gustaaf Eerenstein amesema ukuaji mzuri wa Benki ya CRDB tangu ilipoanzishwa mwaka 1996 unawavutia wawekezaji kuiamini kwani imeweza kukuza mizania yake mpaka kufika thamani ya shilioni trilioni 12.5 sawa na dola za Marekani bilioni 4.9.
“Mkopo huu unadhihirisha ubora wa menejimenti na wafanyakazi wa Benki ya CRDB katika mazingira haya magumu ya biashara tuliyonayo duniani kote ambako biashara nyingi zinayumba kutokana na sababu mbalimbali. Tuna furaha kubwa kuwa sehemu ya wabia wa taasisi hii kubwa ya fedha barani Afrika,” amesema Eerenstein.
Baada ya kusainiwa kwa mkopo huo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Mwambapa amesema fedha zipo hivyo kuwakaribisha wafanyabiashara wakubwa hasa wanaohitaji fedha za kigeni kuitumia fursa hii kuimarisha miradi yao na kuchangia kukuza uchumi wa taifa.
“Benki ya CRDB inawapa kipaumbele vijana na wanawake, fedha hizi pia zipo kwa ajili ya makundi haya muhimu katika uchumi wetu. Napenda kuwahakikishia kwamba tupo tayari kuwahudumia kwa viwango vya kimataifa ili kwa pamoja tuujenge uchumi wetu,” amesema Tully.
Akiwashukuru wadau wote walioshiriki kufanikisha kupatikana kwa fedha hizo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dkt Ally Laay amesema kwa sasa benki hiyo ipo tayari kukidhi mahitaji ya kila mfanyabiashara au mwekezaji nchini.
“Tunao wabia wengi wenye uwezo wa kutusaidia kufanikisha chochote tunachokikusudia. Hivyo tukipata mteja anayetaka fedha nyingi, tunamkaribisha na kwa hakika tutamhudumia kwa viwango vikubwa kutimiza ndoto yake,” amesema Dkt Laay.