Kuelekea kipindi cha mwishoni mwa mwaka jeshi la polisi mkoani Shinyanga limejipanga kuimarisha usalama na kuzuia maandamano na mikusanyiko inayoashiria vurugu ndani ya mkoa wa Shinyanga.
Hayo yamebainishwa leo Oktoba 11, 2023 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP . Janeth Magomi. wakati wa zoezi la utayari kwa jeshi la polisi mkoani humo kuelekea mwishoni mwa mwaka.
Akizungumza mara baada ya zoezi hilo lililoambatana na matembezi ya mataa kwa mataa Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP. Janeth Magomi amebainisha kuwa jeshi la polisi limejipanga kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao na kupiga marufuku maandamano na mikusanyiko inayoashiria vurugu.
"Tumejipanga madhubuti kuhakikisha kuwa tunapo kwenda mwisho wa mwaka tunasimamia jukumu letu la msingi la kulinda usalama wa raia na mali zao, uharifu wa mwisho wa mwaka ikiwemo unyang'anyi wa kutumia nguvu na siraha tutakabiliana nayo na kusimamia usalama", amesema Kamanda Magomi.
Aidha Kamanda Magomi amewataka watumiaji wa vyombo vya usafiri kufuata sheria na taratibu za usalama barabarani lakini pia amepiga marufuku maandamano, mikusanyiko inayoashiria vurugu ndani ya Shinyanga.
"Lakini pia maandamano na mikusanyiko ya aina yoyote inayoashiria vurugu ndani ya Shinyanga vyote tunavikataza na ni marufuku hivyo niwahakikishie watu wa Shinyanga tumejipanga vikosi vyote kuhakikisha tunalinda usalama wa raia na mali zao", aliongeza Kamanda Magomi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi akizungumza mara baada ya zoezi hilo.