WAZIRI GWAJIMA AWAPONGEZA MERK FOUNDATION KUSOMESHA MADAKTARI 42 NCHINI TANZANIA


Waziri Gwajima awapongeza Merck Foundation kusomesha Madaktari 42 NchiniTanzania

Na Marco Maduhu, INDIA

WAZIRI wa Maendeleo ya jamii,jinsia wanawake na makundi maalumu nchini Tanzania Dk.Dorothy Gwajima, ameipongeza Taasisi ya Merck Foundation, kwa kushirikiana na Tanzania na kusomesha Madaktari 42 kwa kuwaongezea ujuzi.

Amebainisha hayo Leo Oktoba 18,2023 Katika Mkutano wa 10 wa Taasisi ya Merck Foundation, na miaka sita ya kampeni ya More than A Mother uliokutanisha wadau kutoka nchi mbalimbali Afrika,wakiwamo na wake wa Marais ambao ni Mabalozi wa kampeni hiyo.
Amesema anawapongeza wadau wa Maendeleo kutoka nchi mbalimbali kuendelea kushirikiana na Tanzania kusukuma gurudumu la Maendeleo Katika Sekta mbalimbali,ikiwamo ya Maendeleo ya Jamii, Afya na hata kutoa vifaa tiba na kusomesha Madaktari.

"Wadau hawa wa Maendeleo Taasisi ya Merck Foundation imekuwa na ushirikiano mzuri na Tanzania, wametusomeshea Madaktari 42 na kuwaongezea ujuzi Katika taaluma zao na kutoa huduma bora ya matibabu kwa wananchi."amesema Waziri Gwajima.
"Madaktari 15 wamesomea ujuzi wa kusaidia wanawake wenye matatizo ya Ugumba, na Madaktari 29 wamesomea Magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwamo Kisukari, Shinikizo la damu na Magonjwa ya Saratani," ameongeza.

Amesema Taasisi hiyo pia imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika masuala ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia,kuwainua wanawake kiuchumi pamoja na kumsomesha Miss Kiziwi (2022) Khadija Kanyama.
Aidha, Waziri Gwajima amempongeza Rais Samia kwa kuifungua Tanzania,na wamekuwa wakishiriki katika Mikutano mbalimbali ya kimataifa na hata kuitangaza nchi Katika masuala mbalimbali ya uwekezaji, utalii na kukuza uchumi.

Amesema Mkutano Mkubwa kama huo wa Merck Foundation utafanyika pia Mwakani nchini Tanzania huko Zanzibar na utaifungua zaidi Tanzania sababu kutakuwa na muingiliano wa watu wengi kutoka nchi mbalimbali Afrika.
Naye mmoja wa Madaktari ambao wamenufaika kusomeshwa na Taasisi ya Merck Foundation Dk.Lucy Mrema kutoka Hospitali ya NIMR Mbeya, amesema amesomea masuala ya Magonjwa ya Kisukari na ameongeza ujuzi Katika utoaji wa matibabu.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Merck Foundation Dk.Rasha Kelej, amesema wataendelea kushirikiana na nchi za Afrika na Mabalozi wa kampeni ya More than A Mother Katika masuala ya kijamii, Afya, kupinga ukatili,unyanyapaa kwa Wagumba, kusomesha watoto wakike,ndoa za utotoni,kwa Maendeleo ya nchi.
Amesema pia wataendelea kuboresha vituo vya Afya,kufanya utafiti wa Kisayansi, pamoja na kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili watumie kalamu zao vizuri kutoa elimu kwa Jamii.
Mkutano huo umehudhuliwa na wadau mbalimbali wakiwamo wake wa Marais kutoka nchi za Angola, Botswana, Burundi, Cabo Verde, Congo, Gambia, Ghana, Liberia, Malawi, Msumbiji, Namibia, Sierra Leone, Zambia,na Zimbabwe.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464