KIKUNDI CHA WAFUGAJI KISHAPU CHAPONGEZWA KUREJESHA MKOPO WOTE WALIOKOPA HALMASHAURI

Kikundi cha umoja ni nguvu cha wafugaji Kishapu chapongezwa kurejesha marejesho ya mkopo waliokopa halmashauri

Na Ofisi ya habari, KISHAPU

AFISA Maendeleo ya jamii wilayani Kishapu Abednego Madole amekipongeza kikundi cha Umoja ni Nguvu cha Wafugaji kilicho Kijiji cha Beledi katika Kata ya Lagana kwa kufanikiwa kurejesha Mkopo wa Sh.4,300,000,ambao walipatiwa na Halmashauri.

Ametoa pongezi hizo jana katika hafla fupi ya kukabidhi Ng'ombe wengine kwa wanakikundi hao.

"Hongereni Sana wanakikundi kwa hatua mliyofikia mmekuwa mfano kwa Vikundi vingine jambo la kumaliza kurejesha mkopo ni jambo kubwa Sana hii inaonyesha ni jinsi mlivyo na uwezo wa kujisimamia endeleeni kujisimamia vyema pamoja na kufata kanuni na Sheria mlizo jiwekea, Halmashauri ipo tayari kushirikiana na nyinyi kupitia ofisi ya Maendeleo ya jamii" amesema Madole.

Aidha, Madole alitumia pia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi kujiunga na mfuko wa bima ya Afya CHF,ili kuwasaidia kupata matibabu hasa pale watakapougua na kukutwa hawana pesa na kutibiwa bure na kuokoa afya zao.

Awali akiwasilisha Taarifa kwa Mgeni Rasmi Katibu wa Kikundi cha Umoja ni Nguvu Bw. Nkuba Shija Masebo, amesema kwamba kikundi kilianza na mtaji wa Sh.75,000 baada ya Hapo walipata mkopo wa Sh. 4,300,000 kutoka Halmashauri ambao uliwasaidia kununua mbuzi 42,na hadi sasa kikundi kina mbuzi 192 Ngo'mbe 9 na Asali mbichi lita 50.

Amesema Kikundi hicho baada ya kurejesha Mkopo wote sasa kimebaki na faida ya Sh.800,000.

Naye Afisa Nyuki kutoka wilayani Kishapu Revocatus Mboya, amekipongeza Kikundi hicho kwa kusimamia nidhamu ya fedha na kujituma katika kuwajibika jambo ambalo watafanikiwa na kuinuka kiuchumi.

"kikundi hiki pia kinajishughulisha na ufugaji wa Nyuki na mimi kama Afisa Nyuki nitawepeni ushirikiano pamoja na kutafuta soko la uhakika kwaajili ya kuuza Asali yenu,"amesema Mboya.

Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Beledi Dotto Izengo ameahidi kutoa ushirikiano kwa kikundi hicho muda wote wanapo hitaji msaada kutoka katika Serikali ya Kijiji,huku akiwapongeza kujikwamua kiuchumi na kuhudumia familia zao na kusomesha watoto.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464