DKT. PHUMZILE MLAMBO – NGCUKA MGENI MAALUM TAMASHA LA JINSIA 2023

 



Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog 

Hayawi hayawi sasa yanaendelea kuwa!! Maandalizi ya Tamasha Maarufu la Jinsia yanazidi kunoga!! Wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania wamethibitisha kushiriki!!

Naam! Ni Tamasha la 15 la Kijinsia linaloratibiwa na Mtandao wa Kijinsia Tanzania TGNP linalotarajiwa kuanza Novemba 7-10,2023 katika Viwanja vya TGNP Jijini Dar es Salaam ambapo Mgeni maalum anatarajiwa kuwa Dkt. Phumile Mlambo - Ngcuka aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la UN Women na Makamu wa Rais wa Afrika Kusini.

Tamasha la Jinsia ambalo limezidi kupata umaarufu siku hadi siku, mwaka huu 2023 linatarajiwa kuhudhuriwa na watu zaidi ya 1500 ambao watatoka nchi mbalimbali wa hapa nchini na kutoka nje ya nchi "Bara la Afrika na mabara mengine".
Lengo kuu la Tamasha la Jinsia ni kupaza sauti za wanawake na kuimarisha ushiriki wao katika lingo za uchumi, jamii, na siasa.

Tamasha la Jinsia linawajumuisha wanaharakati wa haki za wanawake kutoka sehemu mbalimbali katika nafasi huru na rafiki ambapo wanapata wasaa wa kutafakari maendeleo ya Vuguvugu la Ukombozi wa Wanawake Kimapinduzi (VUWaKi), kusherehekea mafanikio na kujulishana changamoto na mikakati mbadala. 

Katika kuimarisha nguvu za pamoja, Tamasha la Jinsia linatayarishwa na TGNP pamoja na Feminist Activist Coalition (FemAct) na taasisi nyingine za kijamii zenye misimamo inayofanana. 

Tamasha la Jinsia linatoa fursa kubwa ya kunoa ajenda ya ufeministi na kujenga muafaka juu ya vipaumbele vya ushawishi katika nyanja za haki za wanawake, uwezeshaji, usawa na haki jamii. 

Pia Tamasha la Jinsia linatoa nafasi adhimu kwa wanaharakati na wana maendeleo kutoka nyanja zote nchini Tanzania, ikiwemo Unguja na Pemba na nchi jirani za Afrika na kwingineko, kujumuika kwa pamoja. 
Hali kadhalika, Washiriki wa Tamasha la Jinsia watajifunza pamoja na kusheherekea mafanikio katika harakati za ukombozi wa mwanamke duniani na Tanzania kwa ujumla  sambamba na kuangalia changamoto zilizojitokeza ndani ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwa TGNP mwaka 1993 hapa nchini na kuangalia namna ambavyo zitatatuliwa.


Dhima ya tamasha hili ni miaka 30 ya TGNP na TAPO la ukombozi wa mwanamke  ambapo dhima hiyo inaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwa TGNP.

Katika tamasha hilo pia kutakuwa na mada mbalimbali zitakazotolewa, wadau watatoa uzoefu wao walivyofanikiwa ikiwa pamoja na kukutanisha watu mbalimbali wa vituo vya maarifa na taarifa kutoka kila mkoa.

JE UNATAKA KUSHIRIKI??



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464