Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango ya Halmashauri ya Kishapu inayoongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kishapu Mhe. William Jijimya imepongeza Miradi inayotekelezwa ndani ya Halmashauri.
Pongezi hizo zimekuja baada ya kukamilisha Ziara ya Kamati ya Fedha iliyofanyika kwa Siku mbili.
Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. William Jijimya akitoa pongezi hizo kwa niaba ya Kamati ya Fedha amesema kwamba Miradi yote inayotekelezwa ipo katika Viwango bora.
"Katika miradi yote ya Maendeleo tuliyopita kwa kweli iko vizuri licha ya kuwa na Changamoto ndogondogo za ubinadamu lakini kazi ni nzuri, pia niawaombe wataalam kuendelea kusimamia Vizuri ili Miradi hii ikamilike katika viwango ambavyo tumekusudia." Alisema Jijimya.
Kwa Upande wake Diwani wa Kata ya Talaga Mhe. Richard Dominick amepongeza miradi inayotekelezwa na Kuziomba kamati za Ujenzi kuzishirikisha jamii ili zitambue miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao.
" Kwa kweli mimi nipongeze kwa jitihada nzuri zinazofanywa na Waalam katika usimamizi wa Ujenzi Miradi ya Maendeleo ipo vizuri sana Ninaomba pia kamati za ujenzi kwa kushirikiana na Wataalam kuzishirikisha jamii ili zitambue Miradi inayotekelezwa ni Mali yao hii itasaidi pia kupunguza wizi mdogo mdogo kwe maeneo ya Ujenzi" alisema Richard.
Naye Afisa Mipango Ndugu Mang'era Mang'era amesema kwamba yupo tayari kuendelea kuhakikisha Miradi yote inayotekelezwa ikamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa ili kuweza kuanzisha miradi mipya.
Aidha Mwenyekiti amewataka Wataalam hasa Idara ya Ujenzi na Mipango kuhakikisha kila Mara wanatembelea miradi inayotekeleza ili kuepusha Miradi kutokukamilika kwa wakati na viwango bora.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464