MADIWANI MANISPAA YA KAHAMA WAMEOMBA KUPUNGUZIWA ANKARA ZA MAJI NA UPATIKANAJI MAENEO YA KATA ZA PEMBEZONI


Kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Kahama Clement Mkusa.

Na Kareny Masasy,Kahama

MADIWANI wa halmashauri ya manispaa ya Kahama  mkoani Shinyanga wameomba kuangalia uwezekano wa kupungua Ankara ya maji  kwa wateja wao na upatikanaji wa maji safi na salama   maeneo ya kwenye kata za pembezoni.

Baadhi ya madiwani hao akiwemo diwani wa kata ya Mondo Kija Peja leo tarehe  20,Septemba,2023 katika kikao cha kawaida cha  baraza la madiwani amesema kijiji cha Mwanzwagi na Mondo vinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji mpaka ilifikia hatua ya kutaka kuifunga shule kwa kukosa maji.

Diwani Peja amesema wananchi unapoitisha mkutano wa hadhara kero yao kubwa ni upatikanaji wa maji  hivyo alitaka kuhakikishiwa na wenye dhamana ya kuwapatia maji ni lini maji watapata wananchi wa maeneo hayo.

Diwani wa kata ya mjini Hamidu Juma amesema  ni bora waelezwe ukweli kwani wananchi wamekuwa wakiwatuhumu madiwani wameshindwa kusikiliza kero zao nakuzitatua  pia kero nyingine ni  Ankara za maji kuwa bei kubwa.

Diwani Juma amesema  serikali ingeleta luku za maji kama ilivyofanya shirika la nishati ya umeme (Tanesco)  kwenye umeme ukiishiwa salio basi lakini sasa Ankara zimekuwa kubwa na baadhi ya wananchi wanashindwa kumudu gharama hizo.

“Suala la kijiji cha Mwanzwagi na Mondo tumeanza kuliongelea muda mrefu kwenye vikao bila kupata ufumbuzi hivyo tunakuomba  mstahiki meya  uwasiliane na Ruwasa kuona nini kinafanyika  majibu ya kufuatilia hayana afya”amesema diwani Juma.

Mstahiki meya wa manispaa hiyo  Yahaya  Bundala amewaomba madiwani  walichukulie suala hili kwa pamoja  ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma  ya maji nzuri.

Kaimu  mkurugenzi wa manispaa hiyo Clement Mkusa amesema suala hilo wamelichukua nakulifanyia kazi.

Afisa mahusiano kutoka mamlaka ya maji Kahama (KUWASA) John Mkama amesema   wako mamlaka mbili ambao wanatekeleza uhitaji wa maji kuna Ruwasa na Kuwasa hivyo maeneo ya  vijijini ni Ruwasa na  wanampango wa bajeti yao.

Mkama amesema kuhusu Ankara ya maji kuwa kubwa  haina uhusiano  na bei  ya maji  hivyo amewaomba madiwani kuendelea kuwaelimisha  wananchi  matumizi  bora ya maji .

"Kuhusu mita za luku katika maji zipo  kwa wateja 25 lakini  bado hazijaleta ufanisi mkubwa  kwa wateja hao na ankara ya  maji kwa uniti moja ni sh 2029 hivyo tujikite kutoa elimu kwa wananchi"amesema Mkama .

Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi  (CCM )wilaya ya
Kahama Thomas Myonga amepongeza kwa madiwani kuibua hoja  na kero  huku akiipongeza serikali kwa kuleta miradi mingi ya maendeleo kama ujenzi wa shule,vituo vya afya na sasa barabara zinaenda kuboresha.





















 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464