Na Mwandishi wetu
MAHAKAMA ya wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga imeanza kusikiliza kesi ya watuhumiwa watatu Raia kutoka nchini India baada ya kukutwa na makosa mbalimbali ikiwemo kuishi nchini bila kibali na kuhujumu uchumi.
Watu hao ni Kerai Dervaj Khmji maarufu babu jii,Nehal Mehta na Jaydeep Kumar Parekh ikiwa walikuwa wakiendesha kampuni ya ununuaji wa madini ya dhahabu iitwayo Nadoyo Minerals Trade Company .
Hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo Edmund Kente leo amesoma shauri la kesi namba 19 ya mwaka 2023 ambapo washtakiwa wote wamekutwa na kosa la kuongoza genge la uhalifu kinyume na aya( 4) (1)( a) ya jedwali la kwanza pamoja na kifungu 57(1) 60 (2) vya sheria ya kuhujumu uchumi ya mwaka 2022.
Hakimu Kente amesema kesi hiyo ni uhujumu uchumi uendeshaji wake kisheria unatakiwa kupata kibali kutoka kwa mwendesha mashtaka mkuu wa serikali (DDP) hivyo imeahirishwa mpaka tarehe 3,Novemba 2023.
Mwendesha mashtaka mkuu wa serikali Yamiko Mlekano akisoma shauri mbele ya washtakiwa hao amesema shitaka la kwanza kuongoza genge la uhalifu,shtaka la pili linamuhsu mtuhumiwa namba moja Kerai Dervaj Khmji kufanya biashara ya madini kinyume cha sheria ya madini.
Mlekamo amesema shtaka la tatu kuisababishia hasara serikali kinyume cha aya 10 (1) jedwali la kwanza pamoja na kifungu 57(1) 60 (2) na shitaka la nne kukutwa na madini kinyume cha sheria cha kifungu 18(1) (4) (a) cha sheria ya madini ya mwaka 2022.
“Wote kwa pamoja wamepelekwa mahabusu bila dhamana kwa mujibu wa sheria ya kesi ya kuhujumu uchumi ya kuisababishia hasara serikali zaidi ya sh Millioni 75.5 kwa kutolipa tozo ya huduma,ada ya ukaguzi na Mrabaha” alisema Mlekamo.
Mlekamo amesema mnamo tarehe 1,Desemba,2022 hadi tarehe 10/Oktoba,2023 wamefanya biashara ya madini bila kibali kwa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga na Mbogwe Mkoani Geita ambapo wameuza madini ya dhahabu gramu 67,310.82 yenye thamani y ash Bilioni 10.5.
Mlekamo amesema shitaka la sita ni utakatishaji wa fedha na shtaka la saba kuingia nchini bila kibali nakuanza kufanya kazi kwa kosa la kifungu cha 45(1) (M) (2) ya sheria ya uhamiaji ya mwaka 2016.
Mshtakiwa wa tatu ambaye ni Jaydeep Kumar Parekh aliingia bila kibali halali cha kuingia nchini mwaka 2021 nakufanya kazi kwenye kampuni hiyo kama mhasibu na mshtakiwa wa pili Nehal Mehta naye kukosa kibali cha kuishi nchini tangu March .2023 na kufanya kazi.
Kesi hiyo imesikilizwa na mawakili wanne wa serikali kwa mara ya kwanza na watuhumiwa wote hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na kesi ya kuhujumu uchumi mpaka pale itakapo tajwa tena.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464