Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme akizungumza na Watendaji wa Vijiji,Kata na Maafisa Tarafa kutoka Halmashauri tatu za Mkoa huo ambazo ni Kishapu,Shinyanga na Manispaa ya Shinyanga
Na Shinyanga Press Club Blog
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga
Christina Mndeme amewaagiza watendaji wa
Vijiji,Kata na maafisa Tarafa kutoka Halmashauri ya Kishapu,Shinyanga na
Manispaa ya Shinyanga kuhakikisha wanakwenda kumaliza migogoro yote ya ardhi
iliyopo kwenye maeneo yao bila kuonea mtu.
Ametoa agizo hilo kwenye kikao kazi kilichowakutanisha watendaji
wa Vijiji,Kata na maafisa Tarafa na kuwaagiza kwenda kusimamia shughuli
mbalimbali kwenye maeneo yao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha migogoro ya ardhi
inakwisha kwa kufuata taratibu.
Kwa upande wa sekta ya maji Mkuu wa Mkoa amesema bado kuna
baadhi ya watu wanalima karibu na vyanzo vya maji na kuharibu miundombinu
ambayo imegharimu fedha nyingi ili kuwasaidia wananchi kupata huduma.
Amewataka kwenda kusimamia na kuhakikisha vyanzo vya maji vyote
na miundombinu yake vinakuwa salama ili vidumu na kuwanufaisha wananchi wengi
zaidi kwa miaka mingi.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme
amewataka watendaji wa Vijiji,Kata na maafisa Tarafa katika Halmashauri zote za
Mkoa huo kusimamia vizuri Fedha za Miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao ili
kuleta tija.
Amesema tangu serikali ya awamu ya sita iingie madarakani Mkoa
wa Shinyanga umepokea Sh Trioni moja kwa ajili ya shughuli za maendeleo na
uendeshaji,Fedha ambazo ni nyingi zinahitaji kuwa na usimamizi mzuri ili
kufikia lengo lililokusudiwa na serikali.
"Nyinyi ndiyo wasimamizi wakubwa wa shughuli za maendeleo
katika maeneo yenu nawaomba nendeni mkaongeze bidii ili kuhakikisha miradi yote
inayotekelezwa inakamilika kwa kiwango na ubora"amesema Mkuu wa Mkoa
Mndeme
Amesema kila mradi unaotekelezwa watendaji wa eneo husika
unawahusu hivyo ni wajibu wao kufuatilia ili kujua kila hatua kwani wao ndiyo
viongozi wa maeneo hayo.
Watendaji wa Vijiji,Kata na Maafisa Tarafa wakiwa kwenye kikao