Na Kareny Masasy,Kahama
MKUU wa mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme amewataka watendaji wa kata,vijiji na mitaa wilayani Kahama kuisemea miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ili wananchi waweze kuifahamu vyema kwenye maeneo yao.
Mndeme ameyasema hayo leo tarehe 19/09/2023 katika kikao kazi na watendaji hao kwa lengo la kuwambusha majukumu ya kusimamia wajibu wao kwa wananchi huku akiwaeleza wao ni watendaji katika sekta zote wanatakiwa kuzifahamu.
Mndeme amesema ingawa wanachangamoto bado kazi wanatenda vizuri hawajakata tamaa na serikali ya awamu ya sita imeona iwashirikishe zaidi ili kuifahamu miradi na waeleze wananchi thamani ya fedha ya miradi hiyo.
“Watendaji jukumu lenu ni kila sekta lililobaya ni ninyi na lililozuri ni ninyi na ndiyo mnamwakilisha Rais kwa kusimamia sekta zote tukiongelea kilimo,Elimu,Afya,Ulinzi na usalama ni ninyi hivyo mmebeba maono ya serikali mnatakiwa mjitambue msiwe chanzo cha kutuhumiwa kwa rushwa”amesema Mndeme.
Mndeme amesema msimu wa kilimo umefika wawasimamie vizuri wakulima wawe na daftari la kumuandika kila mkulima kufahamu idadi ya ekari anazolima,mazao gani analima ili mkoa uwe na takwimu sahihi za wakulima.
“Katika suala la upatikanaji wa mbolea kwa msimu wa mwaka 2023/2024 mpango ni mzuri jumla ya tani 3,278 za mbolea zipo kwa mawakala wanaouza mbolea katika halmashauri zenu hivyo nawahimiza wakulima kwenda kununua mbolea kwa mawakala wanaouza mbolea hizo”amesema Mndeme.
Mndeme amesema hivi sasa watendaji wanapata raha katika utendaji wao vijiji 506 ndani ya mkoa huu vimefikiwa na miradi ya aina tofauti tofauti zamani ujenzi wa vyumba vya madarasa,matundu ya vyoo na madawati upatinaji wake ilikuwa wazazi wanachangia fedha na mpaka kufikia hatua kukosana.
Mndeme
amewataka watendaji pia wawe mstari wa mbele kupinga vitendo vya ukatili kwa
watoto na wanawake ikiwemo kuzuia utoro shuleni na ndoa za wanafunzi,
kutumikishwa watoto na kuwaficha wahamiaji haramu matatizo hayo wayabebe na
kuikomboa jamii.
a
Watendaji kutoka wilaya ya Kahama wakiwa kwenye kikao
Katibu tawala mkoa wa Shinyanga profesa Siza Tumbo akiongea kwenye kikao kazi na watendaji
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme akiongea kwenye kikao kazi na watendaji wa kata,vijiji,na mitaa wilayani Kahama.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464