Na Mwandishi Wetu, Arusha
Kwa mara ya kwanza Tanzania imepata heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano wa masuala ya wanyamapori, kilimo na misitu.
Akiongea na waandishi wa habari leo mara baada ya kufungua mkutano wa 24 wa Kamisheni ya Afrika ya Misitu na Wanyamapori (AFWC24) na wiki ya Nane (08) ya Misitu na Wanyamapori Afrika (AFWW8) jijini Arusha, Waziri wa Maliasili na Utalii mh. Angellah Kairuki amesema hiyo ni heshima kubwa kwani kati ya nchi 53 ambazo ndio wanachama wa kamisheni hiyo, nchi 40 zimetuma wawakilishi wake .
“Hadi sasa tuna washiriki takriban 300 , lakini wapo pia wengine ambao watashiriki kupitia njia ya mtandao. Tunaamini watanufaika lakini hasa sisi Watanzania. Wataalam kutoka serikalini wanao simamia masula haya, tutakuwa pia na majadiliano mahususi kuhusiana na biashara nzima ya hewa ukaa” ,amesema Mhe. Kairuki.
Ameongeza kuwa Wadau wa mkutano huo watajadili soko lililopo pamoja na fursa zinazopatikana ambapo ameipongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kwa kuendelea kufanya majadiliano na wawekezaji wa biashara ya hewa ya ukaa.
Wakati huo huo, Mhe. Kairuki amesema Tanzania imekuwa ikitekeleza Sera ya Wanyamapori Tanzania (2007), inayotaka uhifadhi wa wanyamapori na makazi yao pamoja na matumizi endelevu ya rasilimali za wanyamapori nchini.
“Utekelezaji wa sera hiyo umewezesha mtandao wa maeneo ya hifadhi Tanzania kukua na kufikia Hifadhi za Taifa 21, Eneo 1 la Hifadhi, Mapori ya Akiba 29, Mapori Tengefu 25, Maeneo 22 ya Hifadhi za Wanyamapori” ,amesema.
Katika hatua nyingine , Kairuki amesema Tanzania ilishinda nafasi ya kuwa mwenyeji wa Kongamano la 50 la Apimondia litakalofanyika Jijini Arusha mwaka 2027,hivyo amewakaribisha wadau hao kuhudhuria mkutano huo.
"Kongamano la Apimondia linatarajiwa kuleta washiriki wapatao 6,000. Ningependa kuchukua fursa hii kuwakaribisha katika Kongamano hili muhimu la Apimondia. Wageni hao mara baada ya mkutano huo watapata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya vivutio vya utalii vilivyopo jijini Arusha na vile vilivyopo nje ya jiji la Arusha”, amesisitiza.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kwanza wa mkutano wa 24 wa Kamisheni ya Afrika ya Misitu na Wanyamapori (AFWC24) na wiki ya Nane (08) ya Misitu na Wanyamapori Afrika (AFWW8), Prof. Dos Santos Silayo amesema, lengo la Mkutano huo ni kubadilishana uzoefu wa pamoja ili waweze kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya misitu na nyuki.
“Namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu hassan kwa kuridhia mkutano kufanyika Jijini Arusha. Mkutano una matokeo chanya katika sekta ya utalii, misitu Pamoja na sekta ya wanyamapori hapa nchini hapa nchini”, amesema.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464