TCRS YASIMAMIA KIKAO CHA KUPOKEA NA KUJADILI TAARIFA YA KAMATI ZA PETS KISHAPU

 TCRS YASIMAMIA KIKAO CHA KUPOKEA NA KUJADILI TAARIFA YA KAMATI ZA PETS KISHAPU

Na Frank Mshana,

Changamoto ya baadhi ya Jumuiya za watumia maji  yaani CBWSO Wilayani Kishapu kutowasomea wananchi mapato na matumizi imetajwa kuwa imeanza kupungua baada ya Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na kutoa huduma za kijamii kwa  watu wenye mahitaji ikiwemo kuwezesha jamii kuboresha miundombinu ya usafi na maji katika maeneo yenye changamoto ya ukame  na uhaba wa maji. 

TCRS imeziwezesha kamati za kufuatilia matumizi ya rasilimali za umma katika, uendeshaji wa miradi ya maji wilayani Kishapu Mradi ambao  unafadhiliwa na shirika la Foundation for Civil Society (FCS) na kutekelezwa na shirika la TCRS kwenye vijiji 10 vilivyoko kata 5 za Bubiki, Bupigi, Ukenyenge, Lagana na Mwakipoya.

Mwanamina Mavura ambaye anaratibu mradi wa ‘’UWAZI NA UWAJIBIKAJI’’ unaotekelezwa na shirika la TCRS kwa ufadhili wa Shirika la Foundation For Civil Society (FCS) wilayani Kishapu amesema malengo ya mradi huo ni kuona jamii inawajibika ipasavyo katika kusimamia na kufuatilia bajeti ya sekta ya maji na kuwakumbusha viongozi juu ya uwazi na uwajibikaji katika kusimamia na kulinda miundombinu ya maji ili kuhakikisha kunakuwa na uendelevu na upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama ili kupunguza athari zinazotokana na ukosefu wa maji safi na salama.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria kikao hicho kilichofanyika tarehe 20/10/2023  wakiwemo madiwani na watendaji wa halmashauri ya wilaya wamezungumzia changamoto ya kukatika maji mara kwa mara  hasa kwenye miradi ya maji ya ziwa Victoria na kuziomba mamlaka za maji KASHWASA na RUWASA kufuatilia changamoto hiyo na kupata ufumbuzi wa kudumu ili kutatua kero hiyo ambayo imetajwa kuleta madhara kwenye jamii.

Nao baadhi ya wajumbe wa kamati za PETS wamewashauri viongozi wa jumuia za watumia maji (CBWSO) kushirikiana  na PETS kama timu moja ili kusaidia upatikanaji wa taarifa muhimu wakati wa ufuatiliaji na kuwataka viongozi wa vijiji kuitisha mikutano ya hadhara kusikiliza kero za wananchi na kuwasomea mapato na matumizi ya miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo yao.

Nao baadhi ya viongozi wa kata na vijiji wamezishauri mamlaka za maji kuanza mchakato wa kuleta teknolojia ya kisasa ya malipo ya kabla kwenye Ankara za maji au mfumo wa matumizi ya token ili kutatua changamoto ya 1` ulimbikizaji wa bili za maji haswa kwenye baadhi ya taasisi za Serikali.

Kuhusu malalamiko ya bei za Ankara za maji, kaimu Meneja wa RUWASA wilaya ya Kishapu Mhandisi Christopher Daniel Damas amewashauri wananchi waliopitiwa na mtandao wa maji kujitahidi kuvuta maji majumbani mwao ili idadi ya watumia maji iongezeke huku Afisa Maendeleo wa Wilaya ya Kishapu Bwana Joseph Swalala akionekana kusikitishwa na mwamko mdogo wa wananchi kuunganisha maji majumbani mwao.

Aidha mwezeshaji wa kikao hicho, Bwana Evance Mvamila amewashauri wataalamu wa RUWASA wanapoandaa (design) miradi ya maji kuhakikisha wazingatia malengo ya muda mrefu mbele ya ongezeko la watu kwa lengo la haklikisha miradi ya maji inayojengwa inakidhi idadi ya watumiaji kwa kipindi kirefu.

Baadhi ya Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu  kutoka kata za mradi, hawakubaki nyuma wakati wa mkutano huo na wamesisitiza kuwa uwazi na uwajibikaji ni nguzo muhimu  ya uendeshaji na usimamizi wa miradi ya maji ili kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama na uendelevu wa miradi.

Mwenyekiti wa kamati ya Elimu, Afya na Maji wa halmashauri ya (W) ya Kishapu Bwana Joel Ndetoson ambaye pia alikuwa ni mwenyekiti wa kikao hicho amelipongeza shirika la TCRS kwa kazi kubwa ya kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa Wilaya ya Kishapu zinapungua huku akitoa ushauri kwa CBWSO kudhibiti mapato yatokanayo na mauzo ya maji pamoja na utatuzi wa changamoto zingine zilizojitokeza



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464