wazazi walio hudhuria soma la lishe kwaajili ya watoto wao.
Na Kareny Masasy,
Udumavu ni hali ya mwili wa binadamu uliokosa virutubisho mwilini vinavyotokana na aina mbalimbali ya makundi ya vyakula vinavyopaswa kuliwa nakubaki katika hali ya kutokuwa vizuri kimwili na kiakili.
Nchi 88 duniani zinakabiliwa na tatizo la udumavu kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika la kimataifa la kuhudumiwa watoto (unicef) ikiwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano takribani Milioni 15 wanatatizo la udumavu.
Nchi za Afrika zina viwango vikubwa vya watoto chini ya umri wa miaka mitano kukabiliwa na tatizo la udumavu ikiwa Somalia na Ethiopi ni nchi zinazoongoza pia.
Tatizo la utapiamlo linaweza kuathiri pato la taifa ikiwa nchi ya Ethiopia hupoteza pato la taifa( GDP) kwa asilimia 16 huku nchi ya Uganda hupoteza pato la Taifa kwa asilimia 11.
Utekelezaji wa mpango wa pili jumuishi wa masuala ya lishe hapa Tanzania mwaka 2021/2022-2025/2026 Katibu mkuu ofisi ya waziri mkuu anayeshughulikia masuala ya sera,bunge na uratibu dk Jim Yonazi anasema bado kuna changamoto za viashiria vya udumavu vimeendelea kuongezeka.
“ Idadi ya watoto wenye udumavu kwa tafiti kutoka ofisi ya takwimu nchini (NBS) zinaonyesha kiwango cha udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambacho ndiyo kiashiria kikuu cha utapiamlo kimepungua kutoka asilimia 34 mwaka 2016 hadi asilimia 30 mwaka 2022”anasema dk Yonazi.
Afisa lishe mkoa wa Shinyanga Yusuph Hamis anasema watoto wakiwa na tatizo la udumavu unaathiri pato la familia na taifa sababu shughuli zote za utekelezaji zitasimama ili kuweza kukabiliana na udumavu ikiwa kuuthibiti inawezekana.
“Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2018 na Tanzania Health Demographic Suvey (THDS) kiwango cha udumavu mkoa wa Shinyanga kilikuwa asilimia 32”.anasema Hamis,
“Na sasa utafiti uliofanywa na ofisi ya takwimu taifa (NBS) kiwango cha udumavu kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano kimepungua nakufikia asilimia 27.5.”anasema Hamis.
Hamisi anasema udumavu kwa kipindi cha miaka miwili tangu kutungwa kwa mimba mtoto akishindwa kulishwa vizuri na ubongo wake unakuwa haujakamilika vizuri hata akifikia utu uzima ubongo wake unakuwa haujakaa vyema akielezwa kitu hakuelewi.
“Lazima tuzingatie kuwalisha watoto wetu vyakuka vyenye virutubisho sio kuwapa chakula cha ina moja ambapo watoto mnawasababishia udumavu”anasema Hamis.
Hamis anasema vyakula vya jamii ya wanyama kama samaki,maziwa,mayai ndiyo vyenye madini ya Zinki na Folik Asidi inatakiwa watoto wapatiwe kwa wingi pamoja na mboga za majani.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme anawasihi wazazi kusimamia suala la lishe bora kwa watoto wao ili kuondokane na tatizo la udumavu ambapo kwa sasa ni asilimia 27.5 ikiwa lengo kufika asilimia 0 hilo linawezekana.
“Wazazi wajibu wetu kuhakikisha watoto hasa walio na umri chini ya miaka mitano hadi minane wanapata lishe bora tuondokane na kuwapa vyakula vya aina moja kwa mazoea”anasema Mndeme
Mndeme anasema mkoa wa Shinyanga una kila aina ya vyakula hakuna sababu ya kuendelea kuwa na watoto wenye udumavu hivyo wamuunge mkono Rais wa Jamhuri wa muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anayepigania lishe bora kwa watoto.
Ofisa lishe halmashauri ya Msalala wilayani Kahama Peter Shimba anasema katika halmashauri hiyo udumavu ni asilimia 0.1 ikiwa upatikanaji wa vyakula kwa urahisi upo ila mpangilio ndiyo bado changamoto kwa wazazi.
“Mtoto akipatwa na udumavu mzazi analazimika kutumia gharama kubwa ya matibabu kumrudisha mtoto kwenye hali yake kwani viungo vyake vya mwili vitakuwa ni dhoofu na hakui kimwili na kiakili ”anasema Shimba.
Shimba anasema yupo mtoto mmoja alikuwa na miaka saba lakini alipopimwa uzito akabainika kuwa na kilo nne hali ambayo iliwalazimu wazazi wake waishi naye hospitali kwa uangalizi mpaka pale atakapotengemaa afya yake huku wakiendelea kutoa pesa nyingi za matibabu.
“Ninawashauri wazazi kuwekeza katika makundi matano ya vyakula utaepuka vitu vingi pesa ambazo utaweza kutumia kwenye gharama ya matibabu utawekeza hata kwenye ujenzi wa nyumba au elimu”anasema Shimba.
Shimba anasema halmashauri ya Msalala katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 ilitenga zaidi ya sh Milioni 600 kwaajili ya lishe kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Ofisa kutoka taasisi ya chakula na lishe nchini (TFNC) Zainabu Abdalah anawasihi maafisa lishe wanaopima viashiria vya udumavu kwa watoto watoe elimu ya lishe kwa wazazi nakuwaeleza madhara ya udumavu katika familia na taifa kwa ujumla.
Kampuni ya Sanku na shirika la Gain Tanzania wameshirikiana kwenye mradi wa kuendeleza kupunguza tatizo la udumavu kwa watoto wote kwa kupitia shule 47 za msingi mkoa wa Shinyanga.
Meneja wa mradi kutoka shirika la Gain Tanzania Archand Ngemela anasema mradi huo utahusisha wazazi ili kuweza kufikia malengo ya kutokomeza udumavu.
“Wapo wadau wa kusindika unga ulioongezwa virutubisho vinavyopatikana kirahisi ikiwemo madini ya Foliki asidi ,zinki,madini joto kwenye chumvi na vitamin B-12 kama muongozo wa serikali ulivyosema”anasema Ngemela.
Meneja wa kampuni ya Sanku kanda ya ziwa Erasmus Minja anasema mkoa umeshapata wadau 38 wenye vinu vya kuchanganyia virutubisho vinyunyuzi (52 ) na unga huo utasambazwa kwenye shule 47 zilizolengwa.
Mwalimu wa shule ya msingi Mwakata suzana Malima anasema ujio wa virutubisho hivyo kwa kuchanganya na unga ili kupikwe uji utasaidia wanafunzi hasa waliopo chekechea na darasa kwanza na pili kuepukana na udumavu.
Baadhi ya wazazi wa halmashauri ya Msalala Hokasi Mashenyenye na Hamida Omari wanasema udumavu ni hali ya mwili wa binadamu kutokukua vizuri ila wamejifunza namna ya kumpatia mtoto mchanganyiko wa vyakula.
“Sisi wazazi tumeelewa umuhimu wa kumpa mtoto aina ya makundi ya vyakula tumesisitizwa kuwapatia matunda kwa wingi,maziwa ,samaki na nyama ikiwemo mboga za majani”anasema Omari.
Katika Program Jumuishi ya Taifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM 2021/22-2025/26 ) inaeleza utaratibu wa lishe shuleni ambapo utafiti wa idadi ya watu na afya wa Tanzania na utafiti wa kitaifa wa lishe na miongozo mbalimbali ya lishe haizungumzii namna bora za lishe watoto kati ya umri wa miaka tatu hadi nane.
Wazazi wakiwa na watoto wao katika kliniki inayotembea wakisubiri kupewa elimu ya lishe halmashauri ya Msalala