KAIMU afisa lishe halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga Peter Shimba.
Na Kareny Masasy,
BAADHI ya wazazi wa kata ya Busangi halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga wameshauriwa kuwapatia watoto wao vyakula vyenye mchanganyiko ili kuujenga mwili katika ukuaji,
Elimu ya Lishe imekuwa ikitolewa kila siku na wataalamu wa masuala ya lishe kwa wajawazito na mama wanaonyonyesha pindi wanapohudhuria Zahanati au vituo vya afya.
Magreth Hamis mkazi wa kijiji cha Busangi anasema amejifunza mtoto wake anatakiwa kupatiwa vyakula vyenye mchangayiko hata akimpikia uji uwe unamchanganyiko wa makundi ya vyakula kisiwe cha aina moja.
Prisca Andrea mkazi wa kijiji cha Busangi mwenye mtoto wa miezi 10 anasema nimefundishwa namna ya kumpatia mtoto vyakula vyenye mchanganyiko na wakati mwingine kumpatia matunda na mboga za majani.
“Mtoto wangu ana mwaka mmoja nilikuwa nampatia wakati mwingine hizi juisi za kwenye makopo nimeelezwa sio nzuri kwa mtoto kitu kizuri ni matunda ambayo yatajenga mwili wake”anasema Bakari Omary mkazi wa kijiji hicho.
Mwenyekiti wa kijiji cha Busangi Joshua Jacob anasema amekuwa akihamasisha suala la lishe kwenye mikutano ya hadhara na vikao sababu vyakula vipo kilichokuwa kikitakiwa ni kuwaelekeza namna ya kuwapa watoto wao.
Mtendaji wa kata ya Busangi Evamary Elias anasema kata hiyo ina vijiji vinne,vitongoji 17 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kuna kaya 1899 na wakazi 11,255.
Elias anasema kila robo ya mwaka kunakuwa na mkutano na wazazi wote lengo kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa lishe kwa mujibu wa mkataba waliokuwa wameusaini mwaka jana .
“Tunawafundisha kwa vitendo namna ya makundi matano ya vyakula yalivyo , kuviandaa,kuvipika vyakula na kuwapatia watoto kwa muda upi ili kuwaepusha na udumavu”anasema Elias.
Diwani wa kata ya Busangi Alexander Mihayo anasema suala la lishe limekuwa likiongelewa kwenye mikutano ya hadhara tangu watendaji waliposaini mikataba ya lishe.
“Wananchi wamepata ufahamu mkubwa kuhusiana na lishe ikiwa wajawazito wakihudhuria kliniki huko huko nako elimu inatolewa zaidi”anasema Mihayo.
Kaimu ofisa lishe kutoka halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga Peter Shimba anasema lishe kwa wajawazito na watoto umri chini ya miaka mitano unatakiwa zaidi sababu kuujenga vizuri mwili na ubongo.
“Mzazi
anatakiwa atambue mtoto wake
anakula chakula cha aina gani kabla hajazaliwa na baada ya
kuzaliwa ambapo ataendelea
kunyonyeshwa mara kwa mara
mpaka atakapotimiza umri wa miaka miwili”anasema Shimba.
Shimba anasema mzazi asipozingatia makundi ya vyakula kwa mtoto atakuwa na uzito pungufu na uwiano wa urefu na uzito vinaendana .
“Moja ya kiashiria cha kuangalia hali ya ukuaji mzuri wa mtoto ni urefu na uzito wake ambapo vinamchango mkubwa pia katika ukuaji wa ubongo kwa mtoto”anasema Shimba.
“Ukondefu kwa halmashauri ya Msalala ni asilimia 0.1 na udumavu ni asilimia 0.1”anasema Shimba.
Shimba anasema mtoto anapokuwa kiumri na uzito lazima uongozeke na changamoto ya mtoto kuwa na uzito pungufu ni kukosa vitu muhimu mwilini mwake hivyo inatakiwa mzazi azingatia makundi ya vyakula.
0fisa lishe mkoa wa Shinyanga Yusuph Hamis anasema ukosefu wa madini ya Vitamin mwili unasababisha watoto chini ya miaka mitano kupata utapiamlo ambao unaathiri katika ukuaji wao.
“Lazima tuzingatie kuwalisha watoto wetu vyakuka vyenye virutubisho na katika makundi matano ya vyakula na sio kuwapa chakula cha ina moja ambapo watoto tunawasababishia udumavu”anasema Hamis.
“vipo virutubisho muhimu katika vyakula kama hatuna tabia ya kuwalisha watoto ni hatari mfano madini ya Zinc na Follic Acid ni muhimu na virutubisho vingi viko kwenye mboga za majani na matunda lakini watoto hawapewi”amesema Hamis.
Hamis anasema moja ya viashiria vinavyosumbua mkoa wa Shinyanga ni watoto chini ya umri wa miaka mitano kuwa na tatizo la upungufu wa damu.
Hamis anasema upungufu wa damu kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano kwa mkoa wa Shinyanga ni asilimia 72 ikimaanisha kila watoto 100 watoto 72 wanaviashiria hivyo sababu hupewa chakula cha aina moja kila siku.
Hamisi anasema tatizo hilo huwafanya watoto kupungua kwa uzito sababu hukosa hamu ya kula na mwili kuwa dhoofu muda wote.
Hamisi anasema hali ya lishe kwa mujibu wa utafiti kutoka ofisi ya takwimu nchini (NBS ) kwa mkoa wa Shinyanga kwa watoto ukondefu ni asilimia 1.3.
Katibu mkuu ofisi ya waziri mkuu anayeshughulikia masuala ya sera,bunge na uratibu dk Jim Yonazi anasema utekelezaji wa mpango jumuishi wa pili wa masuala ya lishe wa mwaka 2021-2022-2025-2026 umekuwa na mafanikio makubwa.
“Kutokana na juhudi za pamoja za wadau wa lishe nchini na kupelekea kuimarika kwa kiasi kikubwa kwa hali ya lishe kumefanya kupungua kwa viwango vya utapiamlo kwa baadhi ya viashiria”anasema dk Yonazi.
Dk Yonazi anasema Mafanikio mengine yameonekana kupungua ni kiwango cha ukondefu kutoka asilimia 3.8 mwaka 2016 hadi asilimia 3.5 na uzito pungufu ni asilimia 12.1 kwa mwaka 2022.
Mkuu wa shughuli za lishe kutoka shirika la umoja wa mataifa la kuhudumiwa watoto duniani Unicef Patric codjia anasema wataendelea kuunga kuunga mkono jitihada za serikali katika kuhakikisha masuala ya lishe yanaendelea kuimarika na kuyafikia malengo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464