VIONGOZI WA KIJAMII WAELEZA WALIVYOJIPANGA KUSAIDIA KUKOMESHA UVAMIZI MGODI WA BARRICK NORTH MARA


Magari yakiwa kazini katika mgodi wa North Mara
Rais na Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow, akimkabidhi ufunguo wa gari Mkuu wa Wilaya Tarime, Michael Mtenjele (kulia) lililotolewa na Barrick kwa ajili ya kusaidia shughuli za kufuatilia miradi ya kijamii kwenye Halmashauri ya Wilaya hiyo hivi karibuni

Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele

***
Kutokana na manufaa mbalimbali wanayoyapata Wananchi kutokana na uwekezaji wa kampuni ya Barrick inayoendesha shughuli za uchimbaji wa madini nchini kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni Twiga Minerals.Wazee wa mila, madiwani na wenyeviti wa serikali za vijiji wilayani Tarime, wamesema wamejipanga kuunganisha juhudi katika kukomesha vitendo vilivyoshamiri katika siku za karibuni vya uvamizi Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara uliopo Nyamongo wilayani humo.


Hivi karibuni, Rais na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Kampuni ya Barrick, Mark Bristow, alipokuwa kwenye ziara ya kikazi nchini aliwaomba viongozi wa serikali, kisiasa na kijamii wilayani Tarime kushirikiana na mgodi wa North Mara katika juhudi za kukomesha uvamizi mgodini unaofanywa na makundi ya watu kwa ajili ya wizi wa mawe ya madini vitendo ambavyo vimekuwa vikihatarisha maisha ya watu na kuharibu miundo mbinu ya mgodi,

“Kama ambavyo nimekuwa nikipokea maombi yenu mengi na kuyatekeleza, na mimi nina ombi moja kwenu; ombi langu ni kwa kila mmoja wetu, kwamba tufanye kazi kwa pamoja kutokomeza hii tabia (uvamizi mgodini),” Bristow alisema katika mkutano ambao pia ulihudhuriwa na viongozi hao, mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele.


Katibu wa wazee wa mila wa koo 12 zinazounda kabila la Wakurya wilayani Tarime, Mwita Nyasibora, amedokeza kuwa wameitikia ombi hilo na kwamba kwa sasa wanajipanga kuweka mkakati mahususi wa kulifanyika kazi.“Tunataka tusaidie mgodi usivamiwe, sisi tunatoa rai kwamba watakaobainika watafikishwa kwenye vyombo vya dola kwa ajili ya kuchukuliwa hatua kali za kisheria ,” alisema Nyasibora katika mahojiano wilayani Tarime juzi.


Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalum kutoka Kata ya Nyamwaga, Mariam Mkono, alisema mgodi wa Barrick North Mara, una mchango mkubwa wa kimaendeleo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, hivyo jamii nzima katika halmashauri hiyo inaguswa moja kwa moja na tatizo la uvamizi mgodini.


“Sisi madiwani wa kata tano zilizo jirani na mgodi wa Barrick North Mara tunaibeba changamoto hii ya uvamizi kuipeleka kwenye vikao vya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ili izungumzwe na madiwani wote kwa sababu huo mgodi unachangia maendeleo kwa kiasi kikubwa kwa kulipa ushuru wa huduma (Service Levy) na kutekeleza miradi mingi ya kijamii kupitia fedha za uwajibikaji wa jamii (CSR) kuanzia kwenye vijiji 11 vya kata tano zinazozunguka mgodi hadi kwenye kata 26 za Halmashauri ya Wilaya ya Tarime”,alisema Mkono.


Diwani Mariam, alidokeza kuwa suala la uvamizi mgodini pia litakuwa ajenda ya kudumu kwenye vikao vya Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) iliyoanzishwa na Barrick kwa lengo la kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi wenyeji kutokana na fedha za mpango wa CSR.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyangoto, Mwita Msegi, amesema kuwa wenyeviti wa vijiji vilivyo jirani na mgodi huo wameweka mkakati wa kukemea uvamizi huo sambamba na kuwaeleza wananchi wa maeneo yao ya uongozi madhara ya uhalifu huo.

“Tumeweka mkakati, tunataka tuanze ziara kwenye vijiji vyote vinavyozunguka mgodi kuelimisha wananchi kuhusu madhara ya kufanya uvamizi mgodini pia kufanya mikutano ya hadhara ya wananchi kwa ajili ya kuzungumza na vijana na wazazi, ikiwemo kuwaeleza madhara ya uvamizi mgodini”,alisema Mwita Msegi.

Msegi alisema ili kufanikisha ajenda hii ili kuulinda mgodi ili uendelee kunufaisha wananchi walio wengi na pia ili kuepusha raia wasiendelee kuumina kutokana na vitendo vya uvamizi mgodini watashirikisha viongozi vitongoji, watendaji wa vijiji na kata, madiwani, wazee wa kimila na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya katika utekelezaji wa mkakati huo.

“Uvamizi mgodini una madhara makubwa hata kwa watu wetu wenyewe, utakuta baadhi yao wanakufa na wengine wanapata vilema, na hata mtu anaweza akadondoka wakati anaruka ukuta akadondoka. Kibaya zaidi unakuta mwenzao akipata jiwe watampiga na hata wanaweza wakamuua kama hana nguvu za kujihami, wanatumia pia ubabe. Wanaenda pamoja lakini wakifika kule wanageukana. Hivyo hata wao wenyewe wanakatana mapanga wanaumizana”,alisema Msengi.

Hivi karibuni Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele. Alikaririwa na vyombo vya habari nchini akisema kuwa Serikali itafanya kila jitihada kuhakikisha vitendo vya uvamizi haramu kwenye mgodi huo na migodi mingine vinakomeshwa. “Uvamizi mgodini ni jambo ambalo hatupendezwi nalo. Tutafanya mikutano ya kuelimisha vijana kuachana na vitendo hivi ili wajihusishe kwenye shughuli mbadala kama kilimo badala ya kutegemea uvamizi mgodini,” alifafanua.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464