WATEJA TUPO KWA AJILI YENU - NSSF WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA

   


#Mkurugenzi Mkuu amshukuru mtoa huduma nambari moja nchini Rais Samia, awashukuru pia wanachama na wafanyakazi wa Mfuko, aahidi muendelezo wa huduma bora zaidi

Na MWANDISHI WETU

Ni kishindo! Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umezindua kwa kishindo maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja 2023 katika hafla iliyofanyika Ofisi za Mfuko, Kinondoni jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Mkurugenzi Mkuu, Masha Mshomba.


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo yenye kauli mbiu isemayo ‘Team Service’ lakini kauli mbiu ya Mfuko ni ‘Ushirikiano kwa Huduma Bora’, Mshomba amesema NSSF inaendelea kuthamini, kutambua na kuheshimu michango ya wateja wake kwa kutoa huduma bora kupitia watumishi wenye uweledi na ari ya kufanyakazi.

Mshomba amesema mafanikio ya NSSF yamechangiwa na uwepo wa wanachama hivyo wanaendelea kuthamini uwepo wapo, huku akisisitiza kuwa uongozi madhubuti wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ndie mtoa huduma namba moja hapa nchini, pia umechangia mafanikio ya Mfuko.

“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya kuingia madarakani anaendelea kuhakikisha kuwa Serikali yake inaboresha maisha ya Watanzania kwa kutoa huduma mbalimbali zikiwemo za afya, elimu, miundombinu pamoja na huduma nyingine za kijamii ambazo zinaenda kuimarisha uchumi wa Taifa na wananchi mmoja mmoja,” amesema.

Mshomba amesema mifuko ya hifadhi ya jamii imefarijika kutokana na kazi kubwa inayofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hasa kuhakikisha mifuko inaendelea kufanya vizuri, inakuwa stahamilivu na inafanya majukumu yake ya msingi ikiwemo kulipa mafao mbalimbali ndani ya muda uliowekwa kisheria.
“Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia kwa kuleta ustahamilivu katika sekta ya hifadhi ya jamii na tunamuomba aendelee kutusimamia na kuhakikisha mifuko hii siku zote inatimiza malengo yake makuu,” amesema Mshomba.

Amesema Mfuko unatambua malengo ya wateja wake katika kufanikisha malengo yake ambapo ameahidi kutoa ushirikiano mkubwa kwa wateja ili nao waweze kuendelea kutoa michango yao.

Mshomba amepongeza kazi kubwa inayoendelea kufanywa na Ofisi ya NSSF Kinondoni ambapo katika kipindi kifupi tokea kuanzishwa kwake imeweza kupata mafanikio makubwa hasa katika yale majukumu ya msingi kuandikisha wanachama, kukusanya michango na kulipa mafao mbalimbali.

Naye, Meneja wa NSSF Mkoa wa Kinondoni, Large Materu, amesema katika kipindi cha robo ya mwaka tokea ilipoanzishwa Ofisi hiyo, imefikia malengo yake kwa asilimia 86 huku makusanyo wakifikia zaidi ya asilimia 90, ulipaji wa mafao mbalimbali wamefikia asilimia 90.37 na katika sekta isiyo rasmi wameshavuka lengo walilowekewa kwa kuandsikisha wanachama wengi zaidi.

Kwa upande wake, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Lulu Mengele, amemshukuru Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba ambaye ameendelea kuwafanya wafanyakazi wote wa Mfuko kuwa wamoja na kufanyakazi kwa ushirikiano na upendo huku pia akipongeza mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa na Ofisi ya Kinondioni ndani ya muda mfupi.

Rehema Chuma, Meneja wa Sekta isiyo rasmi, amesema Serikali kupitia NSSF imejipanga kuwafikia Watanzania wengi waliopo katika sekta isiyo rasmi kunufaika na hifadhi ya jamii kwa kujiunga na kuchangia NSSF ambapo kwa sasa Mfuko unaendelea kukamilisha taratibu ili kuuzindua rasmi Mpango wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii kwa Sekta isiyo Rasmi ambao utawavutia wananchi wengi.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464