MWAITEBELE AWATAKA WATUMISHI TRA MKOA WA SHINYANGA KUYAISHI MAADILI


MWAITEBELE AWATAKA WATUMISHI TRA MKOA WA SHINYANGA KUYAISHI MAADILI

KATIBU Msaidizi, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Magharibi Ndg Gerald Mwaitebele ametoa mafunzo haya kwa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania - TRA Mkoa wa Shinyanga huku akiwataka kuanzia sasa kuyaishi maadili haya kwakuwa wao ni watumishi wa umma na kwamba ni kioo kwa umma wanaoutumikia.

Maelekezo haya yametolewa Jana na Mwaitebele katika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi za mamlaka hii mbele ya watumishi wote huku akiwasisitiza kubadilisha tabia, matumizi mabaya ya lugha kwa wanaowahudumia, kuacha kuomba rushwa, kukopa bila kuoipa, kutoa siri za ofisi ili kuihujumu na badala yake wawe waadilifu ndani na nje ya ofisi kwakuwa wao ni viongozi wa umma.

"Kuanzia sasa tubadilishe mwenendo wetu, tubadili tabia zetu, matumizi ya lugha kwa tunaowahudumia ambao ndiyo umma, tuanze kuyaishi maadili kuanzia leo na tukumbuke kuwa sisi ni viongozi tunaotumikia umma hivyo tunatakiwa kuwa kioo mbele ya umma", amesema Mwaitebele.

Kando na hayo Mwaitebele alitaja miongoni mwa sifa na utambulisho wa mtumishi mwadilifu kwa umma ikiwemo pamoja na kujali wengine wakati wote, kujitolea kusaidia wenye uhitaji bila kujali kama anacho au hana, kuwa msikivu, mwaminifu nyakati zote na anayeheshimu kila mtu bila ubaguzi. Sifa nyingine ni pamoja na kuwa mnyenyekevu, kufanya kazi kwa bidii, kutenda haki, anapaswa kufikiria kwa makini kabla ya kutenda, kujizuia na tamaa ya aina yoyote na kuwa tayari na kukubali kukoselewa na kubadilika.

Misingi ya maadili katika Sekta ya umma ni muhimu sana ili kulinda maslahi ya umma na kukuza uwajibikaji kwa umma, sheria ya maadili ya viongozi wa umma, sheria ya utumishi wa umma pamoja na kanuni zake zimeanisha misinhi kadhaa ikiwemo Uadilifu, Haki ya kutopendelea, Kuheshimu sheria, kutopokea zawadi au fadhila kutoka kwa unayemuhudumia, kufanya kazi kwa uwazi zaidi kwa masuala yaliyoruhusiwa kuwa wazi, Uwajibikaji kwa maana ya kufanya kazi kwa ufanisi na kukamilisha kwa wakati.

Misingi mingine ni pamoja na Uaminifu na ukweli ambapo hapa mtumishi anapaswa kuwa na tabia ya kuheshimu dhamana aliyopewa na kuaminika kwa umma na Matumizi sahihi ya taarifa ambapo nyaraka za siri lazima zitunzwe na hazipaswi kutumika kwa manufaa binafsi au kuathiri utendaji kazi, mfano kutoa siri za mikakati ya TRA kwa wateja kwa maslahi yako na uliyempa siri hiyo, kutoa nyaraka za TRA na kumpa mteja au kiongozi wa chama cha kisiasa bila kufuata utaratibu hapo utakuwa umekiuka misingi ya maadili ya utumishi wa umma.

Awali akimkaribisha muwezeshaji, Meneja TRA Mkoa wa Shinyanga Ndg. Faustine C. Mdessa alisema kuwa wao kama watumishi na viongozi wa umma wapo tayari kupokea mafunzo ya maadili ya viongozi wa umma, wapo tayari kupokea maelekezo, miongozo na ushauri wote watakaopewa na kwamba kuanzia sasa wamebadilika na watayaishi maadili ya viongozi wa umma kwa vitendo.

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ni Idara ya Serikali inayojitegemea chini ya Ofisi ya Rais ambayo imepewa jukumu la kusimamia mienendo na tabia ya viongozi wa umma.

Sekretarieti imeanzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995, ambapo Kamishna wa Maadili ndiye Msimamizi Mkuu wa shughuli za Taasisi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464