MGONJWA AFYA YA AKILI AUWA WATOTO WAWILI KWA MAPANGA NAYEYE AUAWA AKITIBIWA KWA MGANGA WA KIENYEJI KISHAPU
Na Marco Maduhu,KISHAPU
MTU Mmoja aliyefahamika kwa jina la Ngani Nyembe (52)mkazi wa kijiji cha Masagala wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, ambaye imeelezwa alipelekwa kutibiwa tatizo la Afya ya akili kwa Mganga wa Kienyeji wilayani humo, amewauwa watoto wawili kwa kuwakata mapanga nayeye kuuawa na wananchi.
Watoto hao ni Asha Said mwenye umri wa miaka 4, na Athuman John mwenye umri wa miaka 2.
Tukio hilo limetokea juzi majira ya saa 7 mchana katika Kijiji cha Mwigumbi Kata ya Mondo wilayani Kishapu, alipokuwa akitibiwa tatizo lake la afya ya akili kwa Mganga wa Kienyeji aliyefahamika kwa jina la John Damila.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi akielezea tukio hilo jana amesema mtu huyo akiwa kwa Mganga huyo akiendelea na matibabu ya afya ya akili, alichukua panga na kuwacharanga watoto wawili waliokuwa jirani na kwa Mganga wakicheza na kupoteza maisha papo hapo.
Amesema baada ya kuwaua watoto hao wananchi wenye hasira kali nao walijichukulia sheria mkononi, na kuanza kumshambuli mtu huyo ambaye nayeye alipoteza maisha papo hapo.
“Watoto wawili ambao wameuwa na mtu huyo mwenye tatizo la Afya ya akili ambaye naye ni Marehemu, ni Asha Saidi mwenye umri wa miaka 4, na Athuman John mwenye umri wa miaka 2,”amesema Magomi.
Aidha, amesema wakati tukio hilo linatokea Mganga huyo wa kienyeji hakuwepo nyumbani bali alikuwa safari, na kubainisha kuwa Jeshi lina msubili arudi ili ajibu tukio hilo pamoja na kutibu mtu mwenye tatizo la afya ya akili bila kibali.
Kamanda pia ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kuendekeza mila potofu na kumpeleka mtu mwenye tatizo la afya ya akili kutibiwa kwa Mganga wa Kienyeji, na wakati Hospitali za watu wenye matatizo kama hayo zipo, na hupatiwa tiba huku wakiwa wamefungiwa katika vyumba maalumu na siyo kuwaacha hadharani.
Diwani wa Kata ya Mondo wilayani Kishapu Wiliam Jijimya alieleza kusikitishwa na tukio hilo, na kuwasihi wananchi wanapokuwa na wagonjwa wawapeleke kwenye huduma za Afya kupata matibabu, na siyo kila kitu kukimbilia kwa Waganga wa Kienyeji.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464