NAIBU WAZIRI KATAMBI: TATHMINI YA KUPIMA UHIMILIVU WA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII INAFANYIKA


MHE. KATAMBI: TATHMINI YA KUPIMA UHIMILIVU WA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII INAFANYIKA.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi amesema Mifuko ya Hifadhi ya Jamii itafanya tathmini ya kupima uhimilivu wake katika hesabu zinazoishia Juni, 2023.

Mhe.Katambi ameyasema hayo Novemba 8, 2023 bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo ambaye amehoji mpango wa serikali wa kufanya mapitio ya malipo ya mkupuo kwenye kanuni mpya ya mafao ya pensheni ya Asilimia 33 kwa wafanyakazi.

Akijibu swali hilo, Mhe.Katambi amesema serikali inatambua umuhimu wa kuboresha mafao ya pensheni ikijumuisha malipo ya mkupuo kwa wafanyakazi na Sheria inaitaka Mifuko kufanya tathimini ya kupima uhimilivu kila baada ya miaka mitatu.

Pia amesema kutoa ushauri na mapendekezo mbalimbali ikijumuisha maboresho ya mafao ya wanachama na kuifanya Mifuko kuwa endelevu.

“Serikali ilitangaza matumizi ya Kanuni mpya ya mafao ya pensheni kuanzia tarehe 1 Julai 2022. Kanuni hiyo iliandaliwa kwa kushirikisha wadau wote (Serikali, Wafanyakazi na Waajiri) kwa lengo la kufanya maboresho ya Pensheni ili kuwianisha mafao ya wanachama na kuifanya Mifuko kuwa endelevu,”amesema.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464