ELIMU YATOLEWA KWA WAJAWAZITO KUTHIBITI KUZALIWA WATOTO MGONGO WAZI NA VICHWA VIKUBWA





Baadhi ya wazazi wakiwa kliniki wakipata elimu juu ya umuhimu wa lishe.

Na Kareny Masasy

WAHUDUMU ngazi ya jamii wamesaidia  uhamasishaji kwa wajawazito kuhakikisha wanafuata taratibu za lishe  ili kuepuka kuzaa watoto wenye changamoto za aina mbalimbali

.

Wakazi wa kijiji cha Kundihili kata ya Ukune halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga   Joyce Kulwa na  Farida Kasikolo  wenye ujauzito wanasema elimu ya lishe wamekuwa wakipatiwa na wahudumu ngazi ya jamii,  kwenye kituo cha afya na   kwenye ofisi ya  mweyekiti wa kijiji.

Mkazi wa kijiji hicho Samson Timoth anasema amekuwa mstari wa mbele kumhamasisha mke wake ambaye anaujauzito wa miezi saba  kweda kliniki kwani wamekuwa wakifundishwa namna ya kumlinda mtoto aliyeko tumboni  kupitia lishe.

Mwenyekiti wa kijiji hicho Makungu Shilunga anasema wenye watoto na wajawazito wanahimizwa kwenda kliniki na wataalamu wa afya kwani wamekuwa wakihudhuria  masomo ya lishe   isitoshe kituo cha afya kipo karibu kimesaidia.

Mtendaji wa kijiji cha Kundihili  Neema Chacha anasema zoezi la utolewaji wa elimu ya lishe limekuwepo kwa kushirikiana na wahudumu ngazi ya jamii ambapo kila robo ya mwaka  wanatoa elimu ya lishe kupitia mkutano wa hadhara.

Chacha anasema wazazi wenye watoto na wajawazito hukusanywa na kupewa elimu ya namna ya kupika na kuvipata vyakula venye virutubishi kwao.

“Kijiji hiki kina kaya 349  na  wakazi  1574 ambapo  mpaka sasa hakuna takwimu ya mama aliyezaa mtoto mweye tatizo la mgongo wazi au kichwa kikubwa kama wapo basi takwimu hiyo ya zamani hata umri wao ni mkubwa kuanzi miaka 10”anasema Chacha.

Ofisa lishe kutoka halmashauri ya Ushetu Hadija Nasibu  anasema mama anakuwa na upungufu wa damu unaotokana na kukosa folic acid mwilini ambayo inasaidia Kwenye utengenezaji mpya wa cells na uzalishwaji wa red blood cells.

Nasibu  anasema   mama aliyekosa folic acid anaweza kuzaa mtoto mwenye mapufungu kama kuzaliwa mgongo wazi au kichwa kikubwa hivyo mama anatakiwa kumeza vidonge vya folic acid kipindi cha miezi 3 ya mwanzo mwamimba.

“Tunajitahidi kutoa elimu kwenye jamii kwa kushirikiana na wahudumu ngazi ya jamii kuanzia kwenye vitongozji  kwa kuwasaka wajawazito kuwapa elimu ya umuhimu wa lishe”anasema Nasibu.

Nasibu anasema upungufu wa madini ya chuma una sababisha kuzalisha kiwango kidogo sana cha damu ndipo mama mjamzito akikosa madini hayo husababisha tatizo kwa mtoto.

Mganga mkuu wa halmashauri ya Ushetu  dk Othman  Matindo anasema kuna wahudumu wa afya ngazi ya jamii zaidi ya 5000 ambao jukumu lao kupita kila kaya yenye watoto na wajawazito kutoa elimu ikiwemo suala la lishe.

 

Ofisa lishe mkoa wa Shinyanga Yusuph Hamis anasema  wapo baadhi ya wajawazito kuwa na tabia ya kufuata mtindo wa maisha wa ulaji  wa kutofuata makundi matano ya  vyakula ambayo ndiyo kichocheo cha kuongeza madini ya Folic acid mwilini.

Ofisa habari  na mawasiliano  kutoka shirika la Child Help Tanzania  Milton Byemerwa anasema madini ya foliki acidi  ni madini yatokanayo  kwenye vyakula vitokanavyo na wanyama kama vile Maziwa, mayai,nyama na samaki na vyakula vya mbogamboga  na matunda.

Byemerwa  anasema mama akikosa madini hayo mwilini anao uwezekano mkubwa wa kuzaa mtoto mwenye ulemavu  wa mgongo wazi na kichwa kikubwa.

Byemerwa  anasema kila mzazi anatamani kuzaa mtoto akiwa na afya njema  lakini tatizo linakuja  mama anapokuwa mjamzito anakosa madini ya foliki acidi.

Byemerwa  anasema  upatikanaji wa vyakula hivyo ni rahisi siyo gharama mama anatakiwa ale  kipindi chote cha  ujauzito na njia nyingine anashauriwa ameze vidonge vyenye madini ya foliki acid  miezi mitatu kabla ya kupata ujauzito.

“Madhara yatokanayo na ukosefu wa viini lishe mwilini  kwa mjamzito anapobahatika kupata mtoto  ndipo linajitokeza tatizo la mgongo wazi,  hutokea kwenye paji la uso,utosini, uti wa mgongo, na kichwa kikubwa”anasema Byemerwa.

Byemerwa anasema   ubongo wa mtoto na mishiba ya fahamu inatengenezwa ndani ya wiki tatu  tangu kutungwa kwa mimba na mama akiwa hana madini ya kutosha mwilini changamoto hujitokeza kwa mtoto anayezaliwa ikiwemo ulemavu.

Byemerwa  anasema wanachokifanya  sasa hivi  kwa watoto wanaozaliwa  ulemavu huo ni kuwatafutia tiba  na kuwaunganisha na madaktari bingwa pamoja na chama cha wazazi wenye watoto wa aina hiyo.

Hapa Tanzania  kwa mujibu  wa  Waziri wa afya Ummy Mwalimu  mwaka jana amesema  watoto zaidi ya   6000 kila mwaka wanazaliwa na tatizo la ulemavu wa aina hiyo.

 “Hapa duniani  vizazi hai  1000  ikiwa wastani watoto  watatu mpaka wanne wanazaliwa na mgongo wazi na  kichwa kikubwa changamoto kubwa ni ukosefu wa lishe kwa mama kabla ya kupata ujauzito”anasema  waziri Ummy.

Ofisa lishe kutoka taasisi ya chakula na lishe nchini (TFNC) Doris Katana anasema Uongezaji virutubishi  maana yake ni kiwango cha kuongeza vitamin au virutubishi kwenye vyakula vya kawaida vinavyopatikana kwenye jamii.

“Lengo kubwa  ni kuboresha hali ya mlaji kwa nia ya  kuzuia na kutibu matatizo ya virutubishi mwilini  hasa  kwa kuanza na  vijana balehe”anasema Katana .

Katana anasema virutubishi hivyo ni madini chuma, vitamin A,  Madini joto lengo kuzuia pale tatizo linapotokea  mfano watu wamekuwa wakitumia mtindo wa maisha  kwenye vyakula vingi ambavyo havina madini.

“Madini ya foliki acidi    ni muhimu kwa mama mwenye umri wa kuzaa  akiwa na upungufu  wa madini hayo hitilafu inatokea na ndipo anampata mtoto mwenye ulemavu huo”Katana .

Katana anasema   ili mama aweze kukaa vizuri hali ya mwili wake wa kujiandaa kupata mtoto  anahitaji  madini hayo yenye  macrogramu 400 kila siku ale matunda,mbogamboga, jamii ya mikunde mayai kwa wingi  nakushauriwa kutumia vidonge vya foliki acidi.

Katika kukabiliana na tatizo la udumavu  nchini waziri mkuu Kassimu Majaliwa amesema serikali inatarajia kutenga  bajeti kwaajili ya ununuzi na usambazaji wa  mashine  maalum za kuchanganya virutubisho kwenye vyakula.

Waziri mkuu Kassimu Majaliwa akikabidhi  mashine zilizotengenezwa  nchini na shirika la Gain  ambapo zitakuwa na kazi ya kuchanganya virutubishi vya vitamin B,Foliki  Acid  sambamba na madini chuma na Zinki kwenye  mahindi wakati wa kusaga.

“Mbinu hiyo itasaidia wanawake kuepuka na changamoto  ya ukosefu wa madini  mbalimbali ambayo yanasababisha mtoto kuzaliwa akiwa na matatizo”anasema  Majaliwa.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464