Na Nyabaganga Taraba - Manyara
Kamati ya kudumu ya Bajeti ya Bunge la Jamhuri ya Tanzania imetembelea mradi wa bwawa la umwagiliaji la Tlawi unaojengwa katika kijiji cha Tlawi kata ya Tlawi,tarafa ya Endagikoti halmashauri ya mji wa Mbulu mkoani Manyara ambapo mradi huo una uwezo wa kumwagilia hekta 90 lakini pia kutunza maji lita Bilioni 10 maji hivyo yanatosha kumwagilia mwaka mzima.
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bajeti ya Bunge la Jamhuri ya Tanzania Mhe. Daniel Sillo amesema Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeridhishwa na utekelezaji wa ujenzi wa mradi bwawa la Tlawi huku akiipongeza Wizara ya Kilimo kwa mradi huo.
Aidha amesema kukamilika kwa mradi huo kuliogharimu bilion 6.4 utakaonufaisha wakulima wa zao la vitunguu swaumu pamoja na mazao mengine utaongeza pato la mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, hivyo mradi huo pamoja na miradi mingine itachangia ongezeko la fedha katika bajeti ya serikali.
Naye Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. David Silinde (MB) amewataka wananchi kutunza mradi huo huku akimpongeza Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Raymond Mndolwa kwa usimamizi thabiti wa miradi ya ujenzi miundombinu ya umwagiliaji.
Silinde pia amewaasa wakulima wa eneo hilo kuutunza na kuulinda mradi huo ili uwe na tija ili kukuza sekta ya umwagiliaji nchini.
Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Raymond Mndolwa amesema Tume itahakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa ambapo hadi sasa mradi umefikia 95% ambapo jumla wakulima 2400 watanufaika.
Mndolwa ameongeza kuwa miradi yote inayojengwa itakamilika kwa wakati na serikali inaendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji.
Wananchi wamemshukuru Rais Samia Suluhu kwa utekelezaji wa miradi ambapo wameeleza kuufurahia mradi na kusema ni sawa na kuongezewa mshahara mara mbili au tatu