MBUNGE SANTIEL KIRUMBA AIOMBA SERIKALI IONGEZE LIKIZO KWA MAMA ALIYEJIFUNGUA MTOTO NJITI




Na Mwandishi wetu – Malunde 1 blog

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga Mhe. Santiel Kirumba ameongoza Maadhimisho ya Mtoto Njiti duniani katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Mkoani Shinyanga huku akiiomba serikali iongeze likizo ya mama aliyejifungua na mtoto njiti.


Maadhimisho hayo ya siku ya Mtoto Njiti Duniani (premature day) yamefanyika katika kituo cha afya Bugarama kilichopo katika kata ya Bugarama Halmashauri ya Msalala ambapo siku ya kimataifa ya watoto njiti huadhimishwa tarehe 17 Novemba kila mwaka ulimwenguni kote kwa nia ya kuelimisha kuhusu kujifungua watoto njiti ambao hawajakomaa na kufikisha wiki 38 (miezi 9).

Maadhimisho hayo yameenda sanjari na kukutana na akina mama wajawazito na mama waliojifungua watoto njiti wanaonyonyesha kuwapa elimu ya kukaa na mtoto njiti sambamba na kugawa majiko ya gesi 50 kwa akina mama hao, watumishi wa afya katika kituo cha afya Bugarama na polisi Jamii.

“Tumegawa majiko ya gesi 50 kwa sekta ya afya inayohusika na mama na mtoto 15, wajawazito 15, akina mama wenye watoto njiti 15, majiko matano yalienda kwa askari polisi wanaohusika na masuala ya ukatili wa kijinsia kwa sababu mama akifanyiwa ukatili wa kijinsia anaweza kujifungua mtoto njiti. Kwa hiyo tumewapongeza polisi jamii kwa kuweza kutupazia sauti na kuchukua hatua haraka. Watumishi wa afya pia tumewapa majiko kuwashukuru kwa mchango wao kwa jinsi wanavyowapigania watoto njiti”, ameeleza Mhe. Santiel Kirumba.


Mhe. Santiel amesema kila mwaka watoto njiti 200,000 wanazaliwa na kutokana na changamoto ambazo watoto njiti wanapitia ni kundi ambalo limesahaulika kutunzwa hasa maeneo ya vijijini wazazi wamekuwa wakipoteza watoto wao kutokana na mazingira duni ya kushindwa kuwatunza.

“Serikali ikiwekeza kidogo tutaona matokeo makubwa, hawa watoto hasa maeneo ya vijijini wamekuwa wakifariki dunia kutokana na kwamba wazazi wao hawawezi kuwatunza, mtoto huyu anatakiwa akae kwenye kangaroo siku 90 tangu azaliwe. Kwa hiyo kwenye hilo unakuta mzazi anashindwa kumhudumia mtoto”,amesema Mhe. Santiel Kirumba.

“Serikali imeanza kufundisha kwenye shule kwamba watoto njiti walelewe, pia Serikali imeweka huduma yam toto njiti kwenye bima, zamani haikuwepo. Kilichobakia ni huduma ya likizo ya uzazi ya mama aliyejifungua mtoto njiti kwa sababu akijifungua ana miezi sita itamtaka akae siku 90 ili mtoto aweze kutimia, lakini tunahitaji huyu mama aongezewe likizo ya uzazi na pia huyu mama apewe benefit anapokuwa katika kulea mtoto njiti kwa sababu kulea mtoto njiti ni gharama na inaweza kumfanya mwanamke arudi nyuma kiuchumi kutokana na kwamba anatumia muda mwingi kumwangalia mtoto zaidi kuliko kufanya shughuli za kumwingizia kipato”,ameongeza Mbunge huyo.

Aidha ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa inazofanya kuboresha sekta ya afya ambapo imeleta shilingi 157 na vifaa tiba na kujenga jengo la mtoto njiti katika mkoa wa Shinyanga.


Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) watoto Milioni 15 duniani huzaliwa kabla ya miezi 9 yaani njiti na hii imekuwa ikiongezeka siku hadi siku hali ambayo inatajwa kuchangia kwa wingi vifo vya watoto chini ya miaka mitano duniani. Kwa mujibu wa WHO kwa kila watoto 10 wanaozaliwa mmoja ni njiti.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga Mhe. Santiel Kirumba akizungumza wakati Maadhimisho ya Mtoto Njiti duniani katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Mkoani Shinyanga Novemba 17,2023
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga Mhe. Santiel Kirumba akimsalimia mmoja wa akina mama katika kituo cha afya Bugarama wakati Maadhimisho ya Mtoto Njiti duniani katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Mkoani Shinyanga Novemba 17,2023






Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464