MWANAFUNZI ASHAWISHIKA KURUDIA DARASA LA NNE AFANYA MTIHANI TENA

Familia ikiwa kwenye mazungumzo ya kumshawishi mwanafunzi aliyegoma kurudia  darasa la nne baada ya kufeli mara ya pili.

Na Kareny Masasy

HATIMAYE  Mwandishi wa habari  na Mwalimu mkuu wa shule hiyo wamefanikisha kumshawishi  mwanafunzi Sara Shija  kuendelea na masomo na kufanya mtihani wa darasa la nne mwezi  Oktoba mwaka huu.

Kugoma kwake kuingia   darasani  kulitokana na matokeo ya  darasa la nne  kutangazwa na kuelezwa kuwa  amefeli mtihani kwa mara ya pili kuingia darasa la tano.

Ambapo viongozi  wa kata ya Lyabukande  halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wameweka mikakati ya kupinga  wanafunzi  kuwa waangalizi wa familia  hali ambayo imewafanya   baadhi yao kuwa watoro wa rejareja shuleni.

Ofisa maendeleo ya jamii kutoka kata hiyo   Salum Mwang'imba  amesema  wakati wa shirika la  Woman Elders Development Organisation (WEADO) linalopinga ukatili   lilifika kutoa elimu juu ya kupinga ukatili  na  kuunda  mabaraza  Saba ya watoto na wanawake.

Mwang'imba amesema  ili kuondoa changamoto hiyo wametoa elimu ya kupinga mila potofu  kwa wazee wa kimila 30 na viongozi wa   sungusungu wa kila kijiji   ambao wamepewa jukumu la kusimamia na  kuweka ajenda ya kudumu kwenye vikao na mikutano  ya hadhara.

"Tumebaini watoto kupewa majukumu ya kulea familia wazazi wao wanakwenda kwenye vibarua  ambapo  wanashindwa kujisomea hata muda wa kupumzika "amesema  Mwang'imba.

Mtendaji wa kata  hiyo Shadrack Malando amesema suala la wanafunzi kuachiwa mzigo wa kulea familia   kipindi cha masomo limetokana  na familia zao hasa ulezi wa upande mmoja.

Mratibu elimu kata Haruni Ibrahimu anasema  kuna vijiji Saba vyote vina shule ya msingi  na shule ya sekondari moja  wameanza kuthibiti utoro kwa kuanza kutoa elimu kwa wanafunzi na wazazi.

Mkurugenzi wa shirika la WEADO  Ananiel Nnko anasema  wanafunzi  kupewa majukumu ya kulea familia ni ukatili mabaraza yaliyoundwa  yatasaidia  kupaza sauti na  kufichua vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa.

 Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi  ya mwaka 2022  kupitia ofisi ya taifa  ya Takwimu (NBS) inaeleza kaya zinaoongozwa na wanawake ni asilimia 35.8  hapa nchini  ikiwa mkoa wa Shinyanga  una asilimia 36.5 juu ya wastani wa kitaifa.

Kaya kuongozwa na wanawake hasa maeneo ya vijijini ndiko  kunawafanya watoto  washindwe kuhudhuria vyema darasani  na kuwapatia majukumu ya kulea familia.

Kaimu ofisa elimu  mkoa   wa Shinyanga  Dedan Rutazika  anasema  watoto wote wenye utoro wa rejareja walihakikisha wanawekewa ulinzi wakutosha kwenye maeneo yao ili  wafikie malengo.

Ambapo Rutazika amesema  kwa shule za msingi upo utoro wa reja reja kwa wanafunzi ikiwa   kuna  wanafunzi 16 ,276  wameripotiwa kuwa na utoro huo kwa mwaka 2023.

Rutazika amesema   utoro huo kuna  wavulana 8497 na wasichana 7779 kwa shule za msingi  672 zilizopo.

 Mwanafunzi akifeli mtihani  wa upimaji  anapewa nafasi  ya  kurudia  darasa hilo na akifaulu anaruhusiwa kuendelea na masomo hivyo wanafunzi anayo nafasi.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464