RAIS WA UTPC- ATOA WITO KWA VYOMBO VYA DOLA KUCHUNGUZA MATUKIO YA UHALIFU KWA WAANDISHI WA HABARI

 






Rais wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari (UTPC), Deogratius Nsokolo.


Na Estomine Henry.

 

Rais wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deogratius Nsokolo ametoa wito kwa vyombo vya dola nchini kuchunguza matukio yote ya uhalifu dhidi ya waandishi wa habari ambayo wamekuwa wakitendewa wakati wakitimiza majukumu yao ya kihabari.

 

Nsokolo ametoa wito huo leo (Novemba 2, 2023), wakati akifungua Mkutano wa siku ya kimataifa ya kukomesha uhalifu dhidi ya waandishi wa habari ambao umefanyika kwa njia ya mtandao (zoom Meeting), ukishirikisha wadau mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari.

 

Amesema kuwa uhalifu dhidi ya waandishi wa habari ni uhalifu kama ulivyo uhalifu mwingine, hivyo UTPC, serikali na wadau wengine, hawana budi kuendelea kuukomesha matukio hayo.

 

Aidha, ameongeza kuwa Uhuru wa vyombo vya habari ni nguzo muhimu katika demokrasia, ambapo Umma unaoheshimu na kuelewa umuhimu wa vyombo vya habari huru unaweza kuchangia katika kudumisha demokrasia thabiti.

 

Amefafanua kuwa Vyombo vya habari vina jukumu la kuchunguza na kutoa taarifa juu ya vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, Kuelimisha umma, kusaidia, kugundua, kusimamia, kuzuia vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu. 

 

‘’Umma ulioelimishwa unaweza kushiriki zaidi katika mchakato wa kisiasa na kijamii na hivyo kuwa na mchango mzuri sana katika ujenzi wa taifa…Kwa kuelewa jukumu la waandishi wa habari katika kuchunguza masuala ya umma, umma unaweza kudai uwazi na uwajibikaji kutoka kwa viongozi wao’’ amesema na kuongeza.anasema Nsokolo

 

‘’Elimu juu ya umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari na jukumu la waandishi wa habari katika jamii ndio dawa peke inayoweza kuchangia katika kujenga jamii yenye habari sahihi, demokrasia imara, na haki za binadamu zinazoheshimiwa na hivyo kujenga taifa, lenye umoja, mshikamano na amani, mambo muhimu katika kuleta maendeleo katika nchi.’’anasema Nsokolo

 

Novemba 2, kila mwaka kuanzia mwaka 2013, Duniani kote huaadhimishwa Siku ya Kimataifa ya kukomesha Uhalifu Dhidi ya Waandishi wa Habari, (International Day to End Impunity for Crimes against Journalists).

 

Kwa mwaka 2023, Maadhimisho haya yanalenga kuongeza uelewa kuhusu changamoto wanazokabiliana nazo waandishi wa habari katika kutekeleza majukumu yao, lakini pia kuonya juu ya kukithiri kwa vitendo vya ukatili na ukandamizaji dhidi ya waandishi wa Habari.

 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464