TANROAD YASEMA DARAJA LA KIGONGO-BUSISI LAFIKIA ASILIMIA 78 ZA UJENZI


TANROAD YASEMA DARAJA LA KIGONGO-BUSISI LAFIKIA ASILIMIA 78 ZA UJENZI
Na Kareny Masasy,

Mwanza

SERIKALI imesimamia ipasavyo ujenzi wa daraja la JP Magufuli (kigongo-Busisi) ambalo ujenzi wake unafanyika mchana na usiku na sasa umefikia asilimia 78 huku wakandarasi wazawa nao wakishiriki kwenye ujenzi huo.

Daraja hilo lenye urefu wa kilomita 3.0 na upana wa mita 28.45 ambalo linaunganisha barabara kuu ya Usagara kwenda wilayani Sengerema mpaka mkoani Geita litakuwa na njia nne mbili kwenda na mbili kurudi.

Meneja wa wakala ya barabara (Tanroads) mkoani Mwanza Mhandisi Paschal Ambrose ameyasema hayo leo tarehe 07,Novemba,2023 mbele ya waandishi wa habari 15 waliokuwa kwenye ziara ya kutembelea mradi huo.

Mhandisi Ambrose amesema mradi huo ulianza kujengwa mwaka 2020 na Rais Samia Suluhu alipochukua madaraka alilikuta likiwa asilimia 25 na kipindi cha miaka miwili kwenye uongozi wake limefikia asilimia 78 mpaka sasa.
Meneja wa wakala ya barabara (Tanroads) mkoani Mwanza Mhandisi Paschal Ambrose akizungumza na vyombo vya habari.“Wasimamizi wakuu wa ujenzi wa daraja hilo ni Tanroads ambapo serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania imegharimu ujenzi huo kwa asilimia 10”amesema Ambrose.

Mhandisi William Sanga kutoka Tanroads mkoani Mwanza amesema zipo sababu zilizopelekea kuchelewa kukamilika ujenzi huo ikiwa vifaa kutoka nchini china vilichelewa, mlipuko wa maambukizi ya virusi vya Corona ,na mwaka 2019 mvua kubwa ilinyesha nakupelekea kina kuwa kirefu cha maji na mradi ukasimama.

“Kwa sasa barabara hii inaunganishwa kwa kutumia vivuko vikubwa vitatu vya Mv Mwanza,Mv Misunguwi na Mv Sengerema inawachukua wananchi takribani masaa mawili kuvuka na kuvusha magari lakini likikamilika waenda kwa miguu watatumia dakika 15 kuvuka na gari dakika tatu”amesema Sanga.

Mhandisi mshauri wa ujenzi daraja hilo Abdulkarimu Majuto amesema daraja hilo limejengwa kwa tekonolojia za kisasa litakuwa na nguzo 67 zilizosimikwa na pande zote za daraja zinaendelea vizuri na malipo yanayofanywa na serikali yanakwenda vizuri.

Wakati huo huo Vicent Tarimo mtaalamu kitengo cha mizani makao makuu Tanroads ametoa elimu kwa waandishi wa habari kuhusu sheria ya jumuiya ya Afrika Mashariki ya udhibiti wa uzito wa magari ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 na kuanza kutumika nchini March Mosi 2019.

George Daffa meneja kitengo usalama barabarani kutoka makao makuu Tanroads amesema barabara zinatumiwa na aina zote za usafiri hivyo amewataka madereva waheshimu alama zilizopo kwani ajali nyingi zinatokea madereva wengi hawatii sheria.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464