WADAU SEKTA YA MAJI WAIPONGEZA RUWASA,WATOA USHAURI



Meneja wa Ruwasa mkoa wa Shinyanga Mhandisi Juliette Payovera

Kareny Masasy,Kahama

WADAU wa sekta ya  maji  wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamepongeza wakala wa maji  na usafi  wa mazingira  vijijini  (Ruwasa)  kwa  kutekeleza  upatikanaji wa maji kwenye maeneo mengi.

Ambapo wadau hao pia  wameshauri  baadhi ya maeneo kuwapatia mtandao wa maji wa visima virefu  na kuwashawishi  wananchi wavute  maji majumbani  mwao  waondokane na utumiaji wa Magati.

Hayo wameyasema leo  tarehe  15,Novemba,2023  kwenye kikao cha wadau wa sekta ya maji  wilayani Kahama  nakuhudhuriwa na taasisi mbalimbali za serikali ikiwemo ofisi ya  bonde la maji ziwa Tanganyika huku mgeni rasmi akiwa mkuu wa wilaya hiyo Mboni Mhita.

Mkuu wa wilaya ya Kahama  Mboni Mhita amesema  Ruwasa wamekuwa wakisimamia vizuri utekelezaji wa miradi ya maji  na sekta hii imekuwa ikitumia gharama kubwa kuliko sekta yoyote  ndiyo maana  utekelezaji unakwenda kwa awamu mradi mmoja unatumia fedha nyingi  na  serikali ya awamu ya sita ndiyo kipaumbele maji.

Diwani wa kata ya Busangi Alexander  Mihayo amesema  maji  yakipatikana kwenye gati  kijiji kimoja  bado haitamsaidia mwananchi kinachotakiwa kuangalia vitongoji viko mbalimbali ni bora mradi wa  visima virefu kila mmoja yatamfikia kwenye kitongoji.

Diwani wakata ya Ulowa  Gabriela Kimaro  amesema  kata hiyo  haina maji hata vyanzo vya maji visima virefu hakuna kutokana na walivyopima wataalamu hawakupata maji ameomba Ruwasa kuharakisha mradi wa maji ziwa Victoria  kwani wananchi wanateseka.

Mwenyekiti wa kamati ya afya, elimu na maji kutoka halmashauri ya Msalala  ambaye ni diwani wa kata ya Segese Joseph  Manyara amesema Ruwasa wafanye utaratibu wa kuzipatia  taasisi kama shule,vituo vya afya ,Zahanati  huduma ya maji  ni muhimu kwani wanateseka maeneo mengine.

Mhasibu wa  CBWSO kutoka  Ukamwana   Masolwa James amesema zipo changamoto za  baadhi yao kutopeleka fedha, shule kutolipa Ankara za maji kwa madai bajeti yao ni ndogo  ila ameipongeza Ruwasa kwa usimamizi mzuri nakufanya fedha kutopotea.

Meneja wa Ruwasa wilaya ya Kahama  mhandisi Paschal Mnyeti amesema  katika bajeti ya mwaka 2022/2023 kuna miradi 14  kwa halmashauri zote tatu za Manispaa ya Kahama ,Ushetu na Msalala na  kutengewa sh Bilioni 21.5 huku CBWSO zikiwa kumi na moja.

 Mhandisi Mnyeti amesema  miradi mingi imeendelea kutekelezwa na mingine imefanyiwa usanifu huku akizitaka CBWSO kutunza jenereta zinazosaidia wao kupata maji pindi  umeme ukikatika ikiwa maeneo mengi hayana umeme na mpango upo wakuwapelekea.

“Mradi wa maji Chona,Bukomera na Ubagwe  upo kwenye utaratibu wa kumpata mkandarasi  ili mradi huo uanze kutekelezwa na ushauri uliotolewa na wadau  wote wamepokea na watafanyia kazi”amesema mhandisi Mnyeti.  

Meneja wa Ruwasa mkoa wa Shinyanga  Mhandisi  Juliette Payovera  amesema  katika bajeti ya mwaka huu  halmashauri ya Ushetu imewekwa kwenye mpango wa kupata maji ya ziwa Victoria  wanachosubiri ni waziri wa  fedha kuidhinisha  na utekelezaji uanze.

“Vyombo vya watoa huduma  ya maji  ngazi ya jamii (CBWSO ) mkoa wa Shinyanga wataanza utaratibu wa kutumia mfumo wa malipo kwa serikali ili kuondoa mwanya  wa upoteaji wa fedha na watapatiwa semina juu ya ulipaji kwa njia hiyo” amesema Mhandisi Payovera.

Mwakilishi wa mkurugenzi  wa bonde  la maji ziwa Tanganyika  Eljah Bachuta  amesema  lazima watu watunze vyanzo vya maji  kwa kuvisimamia vizuri  bila kuweka taka zinazotengeneza sumu kwenye maji,kutotumia kemikali  na kusimamia sheria  na kanuni za usimamizi wa Rasilimali ya maji.

Meneja wa wakala wa vipimo (WMA)  mkoa wa Shinyanga Emmanuel  Malanga  amesema  ipo sheria ya vipimo  sura namba 340 kanuni ya nne  inayotaka  mita ya dira  za maji  lazima kupimwa ili isimpunje mtumiaji au kusababisha hasara.


Mwakilishi wa bonde la maji  ziwa Tanganyika






Meneja Ruwasa wilaya ya Kahama Mhandisi Paschal Mnyeti



Diwani kata ya Busanda Alexander Mihayo akichangia majadala huduma ya maji

Meneja  Ruwasa mkoa wa Shinyanga Juliette Payovera

 Mhasibu  CBWSO  kutoka  Ukamwana  Masolwa James  akiwakilisha namna wamavyo pata huduma  na changamoto zilizopo



Diwani wa kata ya Ikinda Matrida Msoma akichangjia hoja



Diwani wa kata ya Segese Joseph Manyara akichangia hoja

Diwani wa kata ya  Ulowa Gabriela Kimaro akichangia hoja

Mkuu wa wilaya ya  Kahama Mboni Mhita akitoa maelezo kuhusu Ruwasa.

Meneja wa Ruwasa mkoa  Mhandisi Juliette Payovera






Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464