Mwanafunzi agoma kurudia darasa la nne baada ya kufeli
Na Kareny Masasy,
MWANAFUNZI wa darasa la nne shule ya msingi Lyabukande Sara Shija (13) amejikuta akibubujikwa na machozi mbele ya mwalimu mkuu wa shule hiyo akikataa kurudia.
Machozi yake yalikuwa yakimaanisha hataki kuendelea na shule kutokana na kurudia darasa la nne kwa mara ya tatu mfululizo.
Shija anaonekana kuongozana na bibi yake ambaye amekuwa kiongozi wa familia na akimlea nakuja moja kwa moja kwenye ofisi ya mwalimu mkuu.
Shija anasema hataki shule kwani hajui kusoma wala kuandika mpaka sasa licha ya kurudia darasa hilo kwa mara ya tatu sasa.
Bibi yake anayefahamika kwa jina la Nyasoro Sengerema (65) anaanza kujieleza kwa mwalimu ujio wake na mwanafunzi huyo (mwijukuu).
Sengerema anasema amemleta Sara Shija ambaye matokeo ya darasa la nne yalivyotoka nakusikia amefeli amekataa kuja shule.
Sengerema ambaye hajui kusoma wala kuandika anapiga magoti mbele ya mwalimu mkuu kutaka mwijukuu wake aendelee na darasa la Tano.
‘Mwalimu nimekuja mwanafunzi amekataa kuja tena shule baada ya kuona anarudia rudia darasa nimekuja kukuomba muacheni aendelee na darasa la Tano”anasema Sengerema.
Sengerema anasema mwanafunzi huyo amekuwa akitoka nyumbani nakuhudhuria masomo shuleni kila siku sio mtoro.
Sengerema anaulizwa na mkuu wa shule kazi za nyumbani huwa zinafanywa na nani hasa? anajibu huwa anazifanya mwanafunzi huyo kutokana na mama yake kuwa ni mgonjwa wa akili.
Mjomba wa mwanafunzi huyo Juliaus Samweli anasema hakujua kama amefeli mara tatu alijua yuko darasa la sita.
“Leo ndio najua amefeli na yuko darasa la nne lakini hajui kusoma wala kuandika hilo anafahamu pia anautoro wa rejareja”anasema Samweli.
Samweli anatoa ushauri kwa mtoto wake huyo arudie kwani akikaa nyumbani itakuwa rahisi kurubuniwa nakupata mimba za utotoni.
“Serikali iangalie mazingira ya vijijini nitofauti na mjini wawape fursa wa vijijini wanapofeli waendelee na darasa lingine kwani huenda mazingira ndiyo yanayosababisha tofauti na mjini”anasema Samweli..
Mwenyekiti wa kijiji cha Lyabukande Peter Labacha anasema zamani wazazi walikuwa na desturi ya kuwaeleza watoto wao wafanye vibaya mitihani ili wakishindwa wawaozeshe.
“Wanaenda wanabadilika kidogokidogo kwa elimu inayoendelea kutolewa na mashirika yanayopinga vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto”anasema Labacha.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Lyabukande Jeremiah Mashaka anasema shule hiyo ilianzishwa mwaka 1956 imekuwa ikijitahidi kufanya vizuri darasa la nne baadhi ya miaka.
Mashaka anasema mwanafunzi huyo anamfahamu ni kweli amerudia kutokana na kufeli mtihani wa darasa la nne.
Mashaka anasema kurudia kwake ni mara ya tatu sasa kwani alioanza nao darasa la kwanza wako darasa la sita mwaka huu.
Mwalimu Mashaka anamjibu bibi kuwa hawezi kwenda kinyume na sera ya elimu ya kwaka 2014 iliyofanyiwa maboresho mwaka 2016 kuwa mwanafunzi akifeli hawezi kuendelea na darasa lingine.
“Historia ya mtoto huyu sikujua kama anaishi na bibi yake nilijua anaishi na wazazi wake amekuwa na utoro wa rejareja kila mwaka”anasema mwalimu mkuu Mashaka.
Mwalimu mkuu Mashaka anasema wazazi wa kata hii waliowengi hasa wazazi wa kike wanawatumikisha watoto wao wa kike kuwa walezi wa familia nakushindwa kumudu masomo.
Mashaka anasema wanafunzi wa darasa la nne waliosajiliwa kufanya mtihani walikuwa 187 na waliofanya mtihani ni 182 wanafunzi watano hawakufanya mtihani kutokana na utoro.
Mashaka anasema wanafunzi 108 wamefaulu lakini wanafunzi 74 wamefeli kwa mwaka 2022 kati yao wasichana 46 na wavulana ni 28.
Mashaka anasema shule nzima inawanafunzi 1002 na darasa moja linawanafunzi zaidi ya 100 na Mwaka 2021 waliofeli darasa la nne ni wanafunzi 69 wote wakarudia.
Mashaka anasema zaidi ya wanafunzi 10 wengi wakiwa wasichana ndiyo wamerudia mara tatu mfululizo.
Mwalimu anayefundisha darasa la nne Herman Shana anasema mwanafunzi Sara Shija ni mtoro wa rejareja kati ya watoto ambao walipangiwa kufundishwa na wanafunzi wenzao naye ni mmoja wapo.
“Tulifanya hivyo ili kuweza kumsaidia afaulu wengine wamefaulu kwani waliokuwa wamependekezwa kuwakumusha pale waliposahau”anasema Mwalimu Shana.
Mratibu elimu kata ya Lyabukande Haruni Ibrahimu anasema changamoto iliyopo watoto wengi wamefeli darasa la nne.
“Kufeli huko kumetokana na utoro wa rejareja,kukabidhiwa kulea familia na wazazi kuwataka wasaidiwe kazi za mashambani na hawana muda wa kujisomea”anasema Ibrahimu.
Ibrahimu anasema wazazi wamekuwa hawafuatilii taarifa za watoto wao wanasubiri wapate taarifa kutoka kwa walimu.
Ibrahimu anasema utoro mwingi wa rejareja unasababishwa na jiografia la eneo hili wanafunzi kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 15.
Mtendaji wa kata hiyo Shadrack Malando anasema jamii inayoishi kwenye kata hii ni wakulima na wafugaji hivyo hawapendi watoto wao wasome.
Meneja mradi Sabrina Majikata kutoka Shirika la ICS lililopo mkoani Shinyanga lenye mradi uliolenga kuwapati elimu walimu juu ya kuwatambua wanafunzi mazingira wanayotoka ikiwa itasaidia kuwapa mbinu zaidi ya ufaulu.
Sera ya elimu ya mwaka 2014 iliyofanyiwa maboresho mwaka 2016 imeeleza mwanafunzi atakaye feli mtihani wa darasa la nne atarudia mwisho mara tatu.
Aidha ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 hadi 2020 imeeleza kuboresha uratibu wa usimamizi wa stadi za kusoma,kuandika na kuhesabu.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464