RC MNDEME AWATAKA WANANCHI SHINYANGA KUITUNZA MIUNDOMBINU YA BARABARA KWA MAENDELEO ENDELEVU
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme, amewataka wananchi mkoani Shinyanga kuitunza miundombinu ya Barabara kwa maendeleo endelevu, na kuacha kulima kando ya hifadhi za Barabara,kupitisha Mifugo na Kung’oa alama za usalama.
Amebainisha hayo leo Decemba 14, 2023 kwenye Kikao cha Bodi ya Barabara.
Amesema jukumu la kutunza miundombinu ya barabara ni la kila mtu, sababu barabara ni kichocheo kikubwa cha Maendeleo endelevu na ukuaji wa uchumi, na kuwataka wananchi waache kufanya uharibifu wa barabara pamoja na kutupa takataka kwenye Mitaro.
“Nawaomba wananchi wa Mkoa wa Shinyanga muitunze miundombinu ya barabara, muache kufanya shughuli za kilimo kando ya barabara,biashara,kupitisha mifugo, magari mazito na kutupa takataka kwenye mitaro,”amesema Mndeme.
Aidha, amewataka TANROADS pamoja na TARURA katika kipindi hiki cha msimu wa mvua, watenge bajeti za dharura kwa ajili ya matengenezo ya barabara ambazo zimekuwa zikihalibiwa na mvua.
Naye Meneja Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS)Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Mibara Ndirimbi, akisoma taarifa yake, amesema katika mwaka wa fedha 2023/2024 kiasi cha fedha Sh.milioni 10.6 zimetengwa kwa ajili ya matengezo ya barabara na Sh,milioni 2.6 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya barabara.
Meneja Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Oscar Mlekwa, akisoma taarifa yake kwenye kikao hicho, amesema katika mwaka wa fedha 2023/2024 kimetengwa kiasi cha fedha Sh.bilioni 16.7 kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya barabara.
Kikao cha Bodi ya Barabara kikiendelea.