RC MNDEME ATOA SIKU 10 KUKAMILISHWA UJENZI KITUO CHA AFYA USHETU
Na. Shinyanga RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme, ametoa muda wa siku 10 kukamilishwa ujenzi wa Kituo cha Afya Ushetu wilayani Kahama, ili wananchi waanze kupata huduma ya matibabu na kuokoa Afya zao.
Ametoa agizo hilo jana alipotembelea na kukagua Maendeleo ya Ujenzi wa Kituo hicho cha Afya Ushetu.
"Mkurugenzi nakupatia siku 10 tu badala ya siku 21 kukamilisha hatua iliyobakia kwakuwa hapa kuna kila kitu, na hakuna sababu kwanini tusimalize haraka ujenzi wa Kituo hiki cha Afya ili wananchi waanze kunufaika na huduma za matibabu", amesema RC Mndeme.
"Kukamilika kwa kituo hiki cha afya kinakwenda kuboresha huduma za afya na kuwaondolea adha wananchi ya kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 20 kwenda Nyamilangano ambako ndiyo kuna Hospitali ya Halmashauri." ameongeza.
Aidha, ameipongeza Halmashauri ya Ushetu kwa kukamilisha ujenzi wa Wodi ya wanawake ambayo imefikia asilimia 90, huku Wodi ya watoto ikiwa imekamilika kwa asilimia 100.
Huu ni muendelezo wa ziara ya RC Mndeme akitembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya mbaimbali ya maendeleo katika halmashauri za Mkoa wa Shinyanga, ambapo alianzia na halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Ushetu,Msalala na kesho Desemba 13, 2023 atakuwa Manispaa ya Kahama.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464