RC MNDEME AMPONGEZA MKURUGENZI WA USHETU UJENZI JENGO LA UTAWALA
Na. Shinyanga RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme, amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu Bi. Hadija Kabojela kwa kusimamia vizuri Ujenzi wa Jengo la Utawala linalojengwa na Mkandarasi MS / Mzinga Holding Co. Ltd ya Mkoani Morogoro na unasimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) linalogharmu zaidi ya Bilioni 5.
RC Mndeme ametoa pongezi hizo jana alipofika Halmashauri ya Ushetu kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Maendeleo ikiwemo ujenzi wa jengo hili ambalo limefikia asilimia 84 ya ujenzi wake.
"Nakupongeza sana Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu Bi. Hadija Kabojela kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo hapa ushetu ikiwemo ujenzi huu wa jengo la utawala, unafanya kazi nzuri, hongera kwa kazi nzuri",amesema Mndeme.
Kando na pongezi hizi, RC Mndeme amemtaka Mkandarasi kuzingatia ubora wa viwango vya ujenzi, thamani ya fedha, bajeti iliyotengwa na kuzingatia muda uliokubaliwa kwa pande zote mbili ambapo mradi unatakiwa kukamilika ifikapo Juni 05, 2024 ukizingatia kuwa hili ndiyo jengo kubwa zaidi la utawala kwa halmashauri zote 6 za mkoa wa Shinyanga.
Kukamilika kwa mradi huu kunakwenda kuboresha utoaji wa huduma na kwenye mazingira bora na rafiki kwa wananchi wa Halmashauri ya Ushetu, na hata ndiyo malengo ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuimarisha utawala bora kwa wananchi wote.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464