NSSF, CMA WAINGIA MKATABA WA USHIRIKIANO UTAKAOCHOCHEA UTENDAJI WA TAASISI HIZO KATIKA KUWAHUDUMIA WANANCHI


Na MWANDISHI WETU, MOROGORO
Mfuko wa Taifa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umeingia mkataba wa ushirikiano na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), wenye lengo la kuongeza ufanisi baina ya taasisi hizo mbili.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kusaini mkataba huo katika Ofisi za NSSF Mkoani Morogoro, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba amesema ushirikiano huo ni nzuri na utachochea ukuaji wa taasisi hizo pamoja na kuboresha huduma.

"Sisi wote wanaNSSF na CMA tupo chini ya Waziri Mkuu ambapo zote tunasimamia sheria mbili ile ya NSSF na ya CMA, lakini mwisho wa siku sheria zote zina mahusiano kwani zinalenga waajiri na waajiriwa ambao wote tunahusika nao, na ndio maana lazima tushirikiane," amesema Mshomba.

Ametaja faida za uhusiano huo kuwa utachochea ukuaji wa usajili wa waajiri na waajiriwa na pia wataendelea kushirikiana katika mambo mbalimbali ikiwemo uwezeshaji hususan CMA kufahamu vizuri masuala ya hifadhi ya jamii.

Naye, Mkurugenzi wa CMA, Usekelege Mpulla amesema majukumu makuu ya tume hiyo ni kusuluhisha na kuamua migogoro ya kazi Tanzania Bara, huku akibainisha kuwa miongoni mwa madai yanayowasilishwa katika tume hiyo ni pamoja na mwajiri kutowasajili wafanyakazi wake NSSF au kutowasilisha michango yao.

"Pamoja na migogoro mengine tunayoipokea, watu wanapokuja kuleta migogoro ya kikazi mojawapo wadau wetu yaani waajiri na waajiriwa wanakuja kuibua madai ya michango ya NSSF," amesema Mpulla.

Amesema makubaliano waliyosaini yamegusa maeneo matano. Miongoni mwa hayo ni kushirikishana taarifa, kuwa na mkakati wa pamoja wa kufikisha huduma za tume na kukusanya taarifa zitakazoenda NSSF na eneo la tatu ni uwezeshaji wa vikao vya tathimini pamoja na mafunzo ili kuwa na uelewa wa pamoja.

Mpulla amesema kuungana huko kutaleta tija kwa pande zote mbili, kutaleta ufanisi na kustawisha taasisi zote mbili kwa sababu zote zinawahudumia wadau wanaofanana.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464