SHUWASA KUTUMIA MABILIONI YA FEDHA KUBORESHA HUDUMA YA MAJI KWA WANANCHI SHINYANGA
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA),wameendelea kujipanga kwa utoaji wa huduma ya Maji safi na salama kwa wananchi wa Shinyanga, ikiwamo kukopa fedha pamoja na kutumia fedha za wafadhili ili kuboresha utoaji wa huduma hiyo.
Hayo yamebainishwa leo Januari 4,2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA Mhandisi Yusup Katopola, wakati alitoa taarifa ya utoaji wa huduma kwa wananchi wa Shinyanga ndani ya miaka mitatu kuanzia 2020 hadi 2023, chini ya utawala wa Rais Samia Mikakati iliyopo, ili kuboresha utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi.
Amesema Mamlaka hiyo ya Maji kwa sasa imepanua mtandao wa utoaji wa huduma ya maji kwamba licha ya kuhudumia wananchi wa Manispaa ya Shinyanga, wanahudumia pia na Miji ya Tinde, Didia na Iselamagazi wilaya ya Shinyanga, na kutoa huduma ya Maji kwa Wananchi laki 2.8.
Amesema katika uboreshaji wa huduma ya Maji kwa Wananchi, Mamlaka hiyo inatajia kukopa fedha benki kiasi cha Sh.milioni 735, pamoja na kupata fedha Euro Mlioni 76 Sawa na Sh.bilioni 200 fedha za kitanzania, kutoka kwa wafadhili AFD ambao wametoa Euro MiL. 75 na Serikali Euro Milioni Moja.
"Fedha hizi zitatumika kuboresha utoaji wa huduma ya Maji na upatikanaji muda wote sababu tutaboresha pia chanzo chetu cha Maji katika Bwawa la Ning'wa nakupeleka maji kwenye Tangi letu la Maji Old Shinyanga ambalo hupokea Maji ya Ziwa Victoria kutoka (KASHWASA)" amesema Mhandisi Katopola.
"Upatikanaji wa huduma ya Maji mpaka sasa kwa Shinyanga Mjini ni asilimia 92, na pembezoni mwa Mji ni asilimia 58 na miradi hii ambayo tunakwenda kuitekeleza ikikamilika huduma ya Maji maeneo ya Mjini utakuwa asilimia 100 na pembezoni asilimia 95," ameongeza.
Aidha, amesema katika miradi 10 ya Maji ambayo wanaitekeleza kwa wananchi yenye thamani ya Sh.bilioni kwamba miradi 7 imekamilika na kuanza kutoa huduma na iliyosalia 3 inaendelea kukamilishwa.
Katika hatua nyingine amesema Mamlaka hiyo imefanikiwa kupunguza upotevu wa maji kutoka asilimia 26 hadi asilimia 20, pamoja na kupata TUZO ya kudhibiti upotevu huo wa maji na hadi kufikia decemba 2023 wamekuwa na upotevu wa maji asilimia 11.
Amesema Mamlaka hiyo pia imefanikiwa wezi wa maji wapatao 76 na wamelipa faini kiasi cha fedha Sh. Milioni 29.16
Pia ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya kudhibiti upotevu wa maji ili kuepuka ongezeko za bili zao za maji kuwa kubwa.
Nao baadhi ya wananchi wa Shinyanga wamepongeza huduma za maji ambazo zinaendelea kutolewa na Mamlaka hiyo, nakuomba ufanisi uongezeke zaidi ili huduma ya maji isiwe inakosekana bali muda wote maji yawepo na kupongeza juhudi za uboreshaji wa bwawa la Ning’wa na siyo kutegemea maji ya kutoka Ziwa Victoria pekee.