RAIS SAMIA ARIDHIA MRADI WA MAJI ZIWA VICTORIA KUFIKISHWA USHETU


Waziri wa Maji Jumaa Aweso.

Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kuanza kwa utekelezaji wa kufikisha mradi wa maji wa Ziwa Victoria katika Halmashauri ya Ushetu.

Waziri wa Maji Jumaa Aweso ameyasema hayo Jana wakati akizungumza na Wananchi wa Busenda katika Kata ya Chona, wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga.

Waziri Aweso amesema kuwa tayari amefanya mawasiliano na watendaji na tayari tenda ya utekelezaji wa mradi wa maji imeshatangazwa ndani ya siku 30 mkandarasi atakuwa amepatikana na kazi itaanza.

Waziri Aweso amezindua mradi wa maji Busenda ambao umegharimu Sh milioni 3.44 fedha zinazotokana na mpango wa malipo kwa matokeo (PforR) huku akimpongeza Mhandisi wa RUWASA Mkoa wa Shinyanga kwa kusimamia kwa weledi mradi huo.

Aweso amesema kuwa ujenzi wa mradi huo ni kutokana na changamoto ya kukosekana kwa huduma ya maji safi na salama na ya uhakika katika kijiji cha Busenda.

Mbunge wa Jimbo la Ushetu Emmanuel Cherehani amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwani mradi huo utasaidia kumtua ndoo mama kichwani.

Wananchi wapatao 3,551 watanufaika na huduma ya majisafi na salama, Cherehani amempongeza Rais Samia kwa kukubali kutoa fedha za ujenzi wa miradi ya maji katika wilaya ya Kahama.

Cherehani ameitaja changamoto kubwa katika jimbo hilo kuwa ni ukosefu wa maji kwani kata 11 kati ya 20 hazijafikiwa na mradi wa maji hivyo mradi wa maji ya ziwa victoria utakuwa muarobaini wa kadhia hiyo.

Utekelezaji wa mradi wa maji Busenda umefanywa na wataalamu wa ndani wa Ruwasa kwa mfumo wa Force Account ambapo utekelezaji wake ulianza rasmi Machi 10, 2023 na kukamilika Septemba 5, 2023.

SOMA HAPA ZAIDI CHANZO HABARI LEO
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464