WATOTO WATATU WAFARIKI DUNIA KWA KUANGUKIWA NA UKUTA WA NYUMBA WILAYANI KAHAMA MMOJA ANUSURIKA

Watoto watatu wafariki dunia kwa kuangukiwa na ukuta wa nyumba Kahama, Mmoja anusurika

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

WATOTO wa tatu wa familia mbili tofauti ambao ni ndugu wamefariki dunia baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba katika Mtaa wa Zongomela Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga.

Watoto hao ni Shija Mihayo (5), Matha Shabani (7) na Maguzu Shija (5).

Tukio hilo limetokea jana Majira ya saa 11 jioni baada ya nyumba waliokuwemo ya matofari ya tope wakijikinga na mvua,kulowa maji na ukuta kuanguka na kisha kuwaponda na kusababisha vifo vya watoto watatu kumjeruhi mtoto mmoja.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi akizungumza leo na waandishi wa habari kutoa taarifa hiyo, amesema katika nyumba hiyo kulikuwa na watoto wanne, lakini watoto watatu ndiyo waliopoteza maisha na kujeruhiwa mmoja.

Amesema mtoto huyo mmoja ambaye ni majeruhi yeye mwenyewe alimkimbiza Hospitali ya Manispaa ya Kahama kupata matibabu, baada ya kufika eneo la tukio sababu alikuwa wilayani Kahama kikazi, huku watoto wale wengine watatu walikuwa tayari wananchi wamewakimbizwa hospitali,

“Mimi nilikuwa kikazi wilayani Kahama wakati napita kwenye Mtaa huo wa Zongomela wananchi wakanisimamisha kuomba msaada wa kumbeba mtoto mmoja ambaye ni majeruhi Salma Shabani miaka 4 ili kumpeleka hospitali ya Manispaa ya Kahama kupata matibabu ndipo nikapewa taarifa ya tukio hilo ”amesema Magomi.

Ameongeza kuwa alipofika Hospitali na kutaka kuwaona watoto wale wengine watatu ambao wananchi waliwakimbiza,aliwakuta tayari wameshafariki dunia.

Aidha, Kamanda ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari na kulinda watoto wao na kuacha kukaa katika maeneo hatarishi katika msimu huu wa mvua, ikiwamo mabondeni, kwenye mikondo ya maji, ili kuepuka kupata madhara na hata kusababisha vifo.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464