MATUMIZI HOLELA YA DAWA KWA WAJAWAZITO YANAVYOWEKA REHANI AFYA YA MTOTO TUMBONI


MATUMIZI HOLELA YA DAWA KWA WAJAWAZITO YANAVYOWEKA REHANI AFYA YA MTOTO TUMBONI

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MWANAMKE anapokuwa Mjamzito anapaswa kuwa na uangalizi wa hali ya juu, ikiwamo kupewa elimu ya matumizi sahihi ya dawa ambazo huthibitishwa na daktari, ili kusaidia ukuaji wa mtoto tumboni na kutoathiriwa na matumizi holela ya dawa na hata mimba kuharibika.

Mjamzito anapokunywa dawa humfikia mtoto kupitia kondo la uzazi, na kama amekunywa dawa ambazo siyo sahihi hazijathibitishwa na daktari, zinaweza kuleta madhara katika maendeleo ya ukuaji wa mtoto tumboni.

Madhara ya dawa wakati wa ujauzito kwa mtoto

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, dawa nyingi huleta madhara hasa ujauzito unapofikisha miezi mitatu sababu ni kipindi ambacho viungo mbalimbali vya mtoto huanza kutengenezwa, hivyo matumizi holela ya dawa huweza kuathiri uumbaji wake.

Madhara ambayo huweza kupata mtoto kutokana na matumizi holela ya dawa ni kutokua vizuri tumboni, kupata maumbile yasiyo ya kawaida, kudumaa akiwa bado yupo tumboni, kuzaliwa akiwa njiti, kupata utindio wa ubongo, na kufariki akiwa bado tumboni au mimba kuharibika.

Kwa mujibu wa tovuti ya afyaMD(Worlpress.com) zinatajwa dawa ambazo ni hatari kwa Mjamzito, kuwa ni Streptomycin, Tetracycline, Cyclophosphamide, Methotrexate,Kanamycin, Ethanol,Valproic acid, na Phenobarbiral.

Mteknolojia wa dawa kutoka Hospitali ya Rufani mkoani Shinyanga Deogratius Ngofongo, naye anataja baadhi ya dawa ambazo ni hatari kwa wajawazito kuwa ni Asplin, ambayo ni hatari sababu hufanya kazi kama damu imeganda, na kwamba mzunguko wa damu ukija kukaa vizuri na kukutwa Mjamzito ameitumia sana, kuwa kipindi cha kujifungua damu zinaweza kutoka nyingi na hata kupoteza maisha na mtoto.

Anataja dawa nyingine kuwa ni Ciprofloxacin, ambayo ni hatari hasa ujauzito unapokuwa na miezi mitatu, ambayo inapita kwenye mfuko wa uzazi na kuweza kuleta madhara makubwa kwa mtoto.

“Dawa yoyote ni sumu ukiitumia vibaya inaweza kukuletea madhara makubwa mwilini, ushauri kwa wajawazito wasitumie dawa yoyote kabla ya kupata vipimo kutoka kwa wataalamu, na kuelekezwa dawa sahihi ya kutumia ili kumlinda mtoto akiwa bado tumboni,”anasema Ngofongo.

“Mjamzito akitumia dawa kiholela ina madhara makubwa katika ukuaji wa mtoto tumboni, na wakati mwingine mimba inaweza kuharibika na kukosa mtoto, na wasihi wajawazito wapende kuhudhuria Klinik kipindi cha ujauzito wao ili wapate ushauri wa wataalamu juu ya matumizi sahihi ya dawa,”anaongeza Ngofongo.

Elimu Matumizi sahihi ya dawa kwa Wajawazito

Afisa Muuguzi kutoka Hospitali ya Rufani Mkoani Shinyanga Daniel Magina, anasema Wajawazito wote ambao hufika kwenye Hospitali hiyo hupatiwa elimu ya matumizi sahihi ya dawa, kipindi cha ujauzito wao hadi kujifungua kupitia kwenye Kliniki, na kusaidia ukuaji wa mtoto na kuzaliwa akiwa salama na afya njema.

Anasema Mjamzito ambaye ana hudhuria Kliniki hawezi kutumia dawa holela, sababu hupimwa na kuelekezwa dawa ambazo anapaswa kutumia kutokana na hatua ya ujauzito wake au tatizo ambalo lina msumbua, lakini wale ambao hawahudhurii Klinik ndiyo hukumbwa na matatizo hayo ya madhara ya kutumia dawa hovyo.

Mjamzito Hadija Mustapha ambaye amefika kujifungua mtoto katika Hospitali ya Rufani mkoani Shinyanga, anasema tangu kipindi cha ujauzito wake alikuwa hawezi kutumia dawa yoyote mpaka aambiwe na daktari.

“Siwezi kunywa dawa hadi niambiwe na daktari, ni hatari Mjamzito kutumia dawa kiholela, na elimu hii nimeipata hospitali siku ya kwanza ambayo nimehudhuria Klinik, na sasa nipo hapa hospitali kwa ajili ya kujifungua,”anasema Hadija.

Mwanamke mwingine Stella Manumbu, anasema tatizo la Wajawazito kutumia madawa holela lipo hasa katika maeneo ya vijijini, ambapo wengi wao hua hawana elimu kutokana na huduma za afya kuwa mbali, na hivyo kwenda kwenye maduka ya madawa kununua dawa mara baada ya kusikia maumivu na kuitumia bila ya kujua madhara yake.

“Tatizo hili lipo sana maeneo ya vijijini mama mjamzito anaweza kujisikia vibaya akamtuma mumewake kwenye duka la dawa amnunulie dawa ya maumivu, na mwanaume akifika anaomba dawa ya maumivu muuzaji anampatia na hapo hajasema anampelekea Mjamzito, hivyo mama akipewa anameza mwisho wa siku anapatwa na matatizo,”anasema Stella.

Chama cha Wafamasia

Katibu Mkuu kutoka Chama cha Wafamasia Tanzania Benson Katundu, anasema matumizi ya holela ya dawa kwa wajawazito ni tatizo, na hupewa dawa hizo kutoka kwenye maduka ya dawa muhimu au Phamancy kinyume na taratibu, sababu dawa kama Antibiotik lazima ziandikwe na daktari ndipo mgonjwa apewe huduma.

Anasema kwenye Maduka ya dawa au Phamancy hua kuna Wataalamu wa dawa na wamesomea kabisa, laki baadhi yao hua siyo waaminifu, na hata wengine kuweka dukani watu ambao hawajasomea kutoa huduma hiyo, na Mgonjwa au Mjazito akifika kuomba dawa fulani anapewa bila hata ya kuonyesha cheti cha daktari.

“Utaratibu wa utoaji dawa kwenye Maduka ya dawa au Phamancy hasa dawa hizi za Antibiotik lazima mnunuaji aonyeshe cheti kutoka kwa daktari, lakini kutokana na wauzaji kutaka hela wanauza hivyo hivyo bila ya kujali afya ya mtu, nawasihi wauzaji wa madawa wasiuze dawa bila cheti cha daktari,”anasema Katundu.

Anatoa Nasaha kwa Wafamasia ambao wanauza dawa kwenye Phamancy kwamba warudi kuishi kwenye taaluma yao na siyo kutanguliza pesa mbele bali wajali afya za wananchi, wasiuze dawa bila cheti cha daktari au kuuliza tatizo la mgonjwa sababu na wao ni wataalamu, na siyo kuuza dawa kiholela waulize kwanza shida nini na kutoa ushauri.

“Nchi za wezetu mfano Ulaya Mfamasia ni mshauri wa daktari, na Ulaya daktari hawezi kukupa dawa mgonjwa pasipo ushauri kutoka kwa Mfamansia, na kwenye maduka haya ya dawa wapo wataalamu, lakini kwa kutojali baadhi yao huuza dawa holela, tena wengine huweka watu kuuza dawa wasio na taaluma,” anasema Katundu.

Mmoja wa wauzaji wa duka la dawa hapa mkoani Shinyanga ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, anasema katika uuzaji wa dawa siyo wote wanaokuja kununua ni wagonjwa husika, wengine hutuma watu kaninunulie dawa fulani, kumbe dawa hiyo anakwenda kupewa Mjamzito na hatimaye kumletea madhara.

Anasema katika maduka mengi ya dawa ni mara chache sana kumuona Mjamzito amekwenda kununua dawa, wengi hutuma watu wao wa karibu na kuelekezwa akanunue dawa fulani kwa mazoea bila ya kupata vipimo, na kutokana na maduka ya dawa kuwa mengi muuzaji hawezi kuuliza uliza maswali itabidi auze dawa na kuingiza pesa.

“Taratibu za uuzaji dawa ni lazima ufahamu tatizo la mgonjwa au aonyeshe cheti kutoka kwa daktari, lakini siku hizi maduka ya dawa yamejaa kila kona, ukijifanya kuuliza maswali mengi mteja anaondoka ana kwenda duka jingine anapata huduma, wewe unabaki na dawa zako.”anasema muuza dawa.

Mipango ya Serikali kudhibiti matumizi holela ya dawa

Kwa mujibu wa Tovuti ya Wizara ya Afya, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu anasema, Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na tatizo la matumizi holela ya dawa hasa Antibiotik, kwa kuondoa usimamizi wa Maduka ya dawa kutoka Baraza la Famasi, na kupeleka majukumu hayo kwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba TMDA.

Anasema tatizo hilo la matumizi holela ya dawa, linachochewa na baadhi ya Wataalamu ambao wanakwenda kinyume na kanuni na miongozi ya taaluma yao, na kuwataka wahudumu wa Afya, Madaktari na Wafamasia kusimama kwenye taaluma zao na kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya dawa.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464