MKURUGENZI SHINYANGA AMEAGIZA WAZAZI WARUDISHIWE MCHANGO WA SH.80,000/- WALIZOCHANGA KIMAKOSA SHULE YA SEKONDARI YA WASICHANA SHINYANGA
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
MKURUGENZI wa Manispaa ya Shinyanga Alexius Kagunze amemuagiza Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Shinyanga iliyopo maeneo ya Butengwa Kata ya Ndembezi Nurah Kamuntu, kuwarudishia wazazi mchango wa Sh.80,000 ambayo walikuwa wameichanga kimakosa mara ya baada ya kuchanganya uchukuaji fomu ya kujiunga na shule hiyo.
Fomu za kujiunga na Shule hiyo ya Sekondari ya Wasichana Shinyanga, kidato cha kwanza wahatakiwi kutoa mchango wowote ule, isipokuwa kidato cha tano ndiyo wanatakiwa kutoa Sh.80,000, ambapo Sh.65,000 ya uendeshaji wa shule na 15,000 kwa ajili ya Tahadhari, Nembo na Kibari cha Shule.
Amebainisha hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari, kwamba fomu za kujiunga na shule hiyo hazitolewi shuleni bali mitandaoni, na kwamba wakati wazazi wakichukua fomu walichanganya badala ya kuchukua ya kidato cha kwanza, wakachukua ya kidato cha tano ambayo ndiyo ina michango ya Sh.80,000 na kisha kulipa kwenye Akaunti ya Shule.
Aidha, amesema kufuata taarifa iliyochapishwa na Gazeti la NIPASHE Januari 17, 2024 ikionyesha baadhi ya wazazi kulalamika juu ya mchango huo wa Sh.80,000 na wakati Serikali inasema elimu bure, ndipo ikabidi afuatilie kwa kina na kubaini kwamba wazazi walichanganya uchukuaji wa fomu za kujiunga na shule hiyo.
“Nimeshatoa maagizo kiasi cha fedha Sh.milioni 4,475,000 ambazo zilikuwa zimelipwa na wazazi kwa mchango huo wa Sh.80,000 zitolewe kwenye Akaunti na kurudishiwa fedha zao, na tayari baadhi ya wazazi wameshazichukua na wengine kutumiwa kwenye simu zao,”amesema Kagunze.
Amesema licha ya mchango huo wa Sh.80,000 wanafunzi walikuwa wakipokelewa ili kuendelea na masomo huku wengine wakiwa hawana hata sare za shule, na kubainisha kwamba mpaka leo wanafunzi 100 tayari wamesharipoti shule kati ya wanafunzi 143 ambao wamepangiwa kujiunga na shule hiyo.
Mkuu wa Shule hiyo ya Sekondari ya Wasichana Shinyanga Nurah Kamuntu, amesema baadhi ya wazazi wamesharudishiwa fedha zao Sh.80,000 na ambao wapo karibu wanachukua mkononi na waliopo mbali wanatumia kwenye simu zao.
Naye Mmoja wa Wazazi Ibrahimu Lyanga, amekiri kuchukua fedha yake Sh.80,000 na kuishukuru Serikali kwa utoaji wa elimu bure.
Mwaka 2016 Serikali ipoanza kutekeleza mpango wa utoaji elimu bure ilifuta Ada na michango yote shuleni kuanzia darasa la Awali hadi kidato cha Nne, na imekuwa ikigharamikia elimu bila malipo takribani Sh.bilioni 23 kila mwezi.
Mwaka 2022 mwezi juni, aliyekuwa Waziri wa fedha na Mipango wakati huo Dk Mwigulu Nchemba alipokuwa akiwasilisha makadirio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23, alipendekeza kufutwa kwa Ada kwa wanafunzi wa kidato cha Tano na Sita ili kuwapunguzia gharama, pendekezo ambalo lilipitishwa na Bunge.